(Na Magreth Kinabo ,MAELEZO Dodoma)
KAMATI ya Uongozi wa Baraza la Vyama vya Siasa inawaomba wajumbe wote wa Bunge Maalum la Katiba kuzingatia kanuni kwani zinakataza vitendo vya utovu wa nidhamu wakati wa vikao vya Bunge hilo .
Kauli hiyo imetolewa leo mjini na Mwenyekiti wa Baraza hilo, Peter Mziray katika mkutano na waandishi wa habari uliofanyika kwenye ukumbi wa Bunge mjini Dodoma kufutia baadhi ya wajumbe wa Bunge hilo kuonesha vitendo visivyo na nidhamu ikiwemo kuzomea.
“ Kamati ya Uongozi wa Baraza la Vyama vya Siasa inawaasa wajumbe wote wa Bunge Maalum la Katiba kubadilika na kuonesha nidamu ambayo Watanzania wote wanategemea kutoka kwao,” alisema Mziray.
Alisema Kamati hiyo inaamini kuwa mjumbe anaweza kutoa hoja yake nzito ya kukubali na kupinga jambo ikakubalika au kukataliwa na wajumbe wengine wengine au Mwenyekiti bila ya kuzomewa.
Aidha Mwenyekiti huyo Mziray amemtaka Mwenyekiti wa Bunge Maalum kutoyatambua makundi ya Tanzania Kwanza na UKAWA kwa kuwa sio makundi rasimu ndani ya Bunge hilo na ndio yanasababisha vurugu kwa kuweka maslahi ya vya siasa mbele badala ya Taifa.
Amewataka wajumbe wa Bunge Maalum la Katiba kuacha kujihusisha na makundi hayo badala yake wachambue na kuunga mkono hoja kwa uzito wa hoja na kuzingatia masilahi ya taifa badala ya kuzingatia mtazamo wa kundi fulani.
Mziray ameongeza kuwa wajumbe wanatakiwa kuepuka vitendo ambavyo vinakwamisha mchakato wa kupata Katiba mpya kwa mustakabali wa taifa hili na Wananchi kwa ujumla.
Katika hatua nyingine Mwenyekiti huyo amesema kuwa Kamati ya Uongozi imeona ni vema wajumbe wa baraza hilo, wakuu wa vyama vya siasa, ambao si wajumbe wa baraza hilo wakutane ili kujadiliana, kushauriana na kuridhiana ili kuweza kufanikisha azma ya kupatikana kwa Katiba Mpya kwa mwafaka.