Majina ya Kamati ya Uongozi Bunge la Katiba Yatajwa, Prof Lipumba Akataa Uteuzi…!
Na Magreth Kinabo, Maelezo Dodoma
Na Magreth Kinabo, Dodoma
MWENYEKITI wa Bunge Maalum la Katiba, Samwel Sitta, ametangaza majina ya wenyeviti na makamu wenyeviti wa Kamati za bunge hilo. Majina hayo yametangazwa na Mwenyekiti huyo baada ya uchaguzi wa viiongozi hao uliofanyika Machi 24, mwaka 2014 mjini Dodoma.
Mwenyekiti ametangaza majina haya baada ya kuunda kamati hizo kwa mujibu wa kanuni ya 54 (1) ya kanuni za Bunge Maalum za Mwaka 2014 ambazo zimetungwa chini ya kifungu cha 26 (1) cha sheria ya Mabadiliko ya Katiba sura ya 83, ambazo zinataja kuundwa kwa kamati 12 za Bunge Maalum.
Wenyeviti na makamu wenyeviti waliochaguliwa katika kamati hizo ni pamoja na Kamati ya Uandishi ambayo Mwenyekiti amechaguliwa, Andrew Chenge, Makamu wake ni Mgeni Hassan Juma. Kamati ya Kanuni Mwenyekiti ni Pandu Ameri Kificho, Makamu wake ni Dk. Susan Kolimba. Kamati Na. 1 Mwenyekiti ni Ummy Ally Mwalimu, na Makamu wake ni Prof. Makame Mbalawa
Wengine waliochaguliwa katika Kamati Na. 2 ni Shamsi Vuai Nahodha ambapo Makamu wake ni Shamsa Mwangunga, Kamati Na. 3 Mwenyekiti ni Dk. Francis Michael, Makamu wake ni Fatma Mussa Juma.
Sitta alisema waliochaguliwa katika Kamati Na. 4 Mwenyekiti ni Christopher Ole-Sendeka, Makamu wake ni Dk. Sira Ubwa Mamboya, Kamati Na. 5 Mwenyekiti ni Hamad Rashid Mohamed Makamu wake ni Assumpter Mshama.
Waliochaguliwa katika Kamati Na. 6 Mwenyekiti ni Stephen Wassira na Makamu wake ni Dk. Maua Daftari, Kamati Na. 7 Mwenyekiti Brig. Hassan Ngwilizi, Makamu wake Waride BakariJabu, Kamati Na. 8 Mwenyekiti ni Job Ndugai, Makamu wake ni Biubwa Yahya Othman.
Hali kadharika Kamati Na. 9 Mwenyekiti ni Kidawa Hamidi Saleh, Makamu wake Wiliam Ngeleja, Kamati Na. 10 Mwenyekiti ni Anna Abdallah, Makamu wake ni Salmin Awadh Salmin, Kamati Na. 11 Mwenyekiti ni Anne Malecela, Makamu wake Hamad Masauni na Kamati Na. 12 Mwenyekiti niwake Paul Kimiti na Makamu wake ni Thuwaybah E. Kisasi.
Aidha, kwa uchaguzi huo, Sitta alitangaza wajumbe wa Kamati ya Uongozi ya Bunge Maalum la Katiba ambao ni wenyekiti wote wa kamati hizo wakiwemo wajumbe wengine watano aliowateua kwa mujibu wa Kanuni.
Wajumbe hao walioteuliwa na Sitta kuingia katika kamati hiyo ni pamoja na Fakharia Khamisi Shomari, Mary Chatanda, Profesa Ibrahim Lipumba, Amon Mpanju na Hamoud Abuu Juma. Hata hivyo pamoja na majina hayo kutangazwa Profesa Lipumba alisimama na kujitoa katika nafasi hiyo hivyo kufanya nafasi za uteuzi kuwa nne badala ya Tano.