Na Veronica Kazimoto, Morogoro
WAMILIKI wa viwanda nchini wameagizwa kutoa taarifa sahihi na ushirikiano wa kutosha wakati wadadisi watakapofika katika ofisi zao kuwahoji kwa ajili ya kupata takwimu za viwanda vyao. Akizungumza wakati wa ufunguzi wa mafunzo ya wadadisi na wasimamisi wa zoezi la Sensa ya Viwanda iliyofanyika mkoani Mororgoro, Naibu Waziri wa Viwanda na Biashara, Janeth Mbene (Mb) amesema ni muhimu wamiliki wa viwanda kutoa ushirikiano wa kutosha kwa wadadisi kwa kuwa takwimu zitakazopatikana kutokana na Sensa hiyo zitatumika katika kupanga shughuli mbalimbali za maendeleo.
“Nichukue Fursa hii kuwaagiza wenye viwanda wote nchini kuona kuwa zoezi hili ni lao na ni jukumu lao kutoa taarifa sahihi kwa wadadisi na pia waone kuwa zoezi hili ni kwa ajili ya manufaa yao na taifa kwa ujumla,” alisema Naibu Waziri Mbene.
Naibu Waziri Mbene amefafanua kuwa, zoezi hili la Sensa ya Viwanda lisichukuliwe kama njia ya Serikali kutaka kujua mapato au faida wanayopata wenye viwanda kwa lengo la kukusanya kodi bali ni kuisaidia Serikali kubaini mabadiliko ya muundo wa sekta ya viwanda, mchango wake kwenye pato la taifa na hatimaye kufanya maamuzi sahihi ya kisera.
Aidha ametoa wito kwa wadadisi wote wanaoshiriki katika mafunzo ya Sensa ya Viwanda kufuatilia na kuzingatia kwa makini mafunzo yote yatakayotolewa na wakufunzi ili lengo la kupata takwimu sahihi za viwanda liweze kufanikiwa. Awali akitoa maelezo ya utangulizi Mkurugenzi Mkuu wa Ofisi ya Taifa ya takwimu Dk. Albina Chuwa amesema takwimu zitakazokusanywa katika Sensa hiyo zitahusu viwanda vidogo, vya kati na vikubwa.
Dk. Chuwa amefafanua kuwa katika sensa hiyo baadhi ya taarifa zitakazokusanywa ni pamoja na anuani na mahali viwanda vilipo, aina ya umiliki, utaifa wa mmiliki, mwaka kiwanda kilipoanzishwa, aina ya bidhaa zinazozalishwa na idadi ya wafanyakazi.
Taarifa nyingine ni gharama za malipo mbalimbali kwa wafanyakazi, mapato yanayotokana na uzalishaji, gharama za uzalishaji na mapato mangineyo.
Mafunzo ya zoezi la Sensa ya Viwanda yamelenga vijana wapatao 175 ambao watafanya kazi ya kukusanya takwimu zinazohusu sekta ya viwanda hapa nchini kwa muda wa miezi miwili kuanzia mwezi Aprili mpaka Juni 2014.