Wabunge Bunge la Katiba Wasema JK Hajavuruga Mchakato wa Katiba

Mwenyekiti wa Wajumbe wa Bunge Maalum la Katiba la Tanzania Kwanza, Said Nkumba (kushoto aliyesimama) akizungumza.

Mwenyekiti wa Wajumbe wa Bunge Maalum la Katiba la Tanzania Kwanza, Said Nkumba (kushoto aliyesimama) akizungumza.


Na Magreth Kinabo – Maelezo, Dodoma
 
UMOJA wa Wajumbe wa Bunge Maalum la Katiba la Tanzania Kwanza umesema kuwa hotuba ya Rais, Jakaya Kikwete aliyoitoa wakati wa uzinduzi wa Bunge Maalum la Katiba hivi karibuni, haikuingilia wala kuvuruga mchakato wa kupata Katiba Mpya, bali kiongozi huyo alitoa maoni na ushauri kama kiongozi wa nchi.

Aidha wajumbe hao wamesema Rais Kikwete hakuingilia kanuni za bunge hilo zilizopitishwa, hakubadilisha Sheria ya Mabadiliko ya Katiba na hakupiga kura kwenye vifungu vya Katiba. Kauli hiyo imetolewa na Mwenyekiti wa wajumbe hao, Said Nkumba alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari kwenye ukumbi wa waandishi wa habari wa Bunge mjini Dodoma.

Nkumba ambaye katika mkutano huo aliambatana na baadhi ya wajumbe wengine watano, alisema hotuba hiyo imeweka wazi faida na hasara za mifumo yote ya Muungano wa Tanzania kwa hoja ili Watanzania wawe na fursa pana ya kutafakari kabla ya kufanya uamuzi.

“Rais ametimiza kauli yake ya kushawishi kwa hoja na si kulazimisha,” alisema Nkumba. Aliongeza kuwa alichokifanya rais katika hotuba yake ni kama kiongozi mkuu wa nchi mwenye hekima na busara na uchungu wa nchi yake na kutambua dhamana aliyopewa na Watanzania wote bila kujali makundi kwa kuelezea faida na hasara za mifumo ya Serikali iliyowasilishwa kwenye hotuba ya Mwenyekiti wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, Jaji Warioba.

“Rais katupa moyo na kutuhimiza tumalize kazi haraka na tuifanye kwa weledi huku tukiweka maslahi ya taifa mbele. Hata pale alipotoa maoni na ushauri kuhusu baadhi ya vifungu bado alisisitiza kwamba umamuzi wa mwisho ni wetu sisi wajumbe wa Bunge Maalum la Katiba,” alisisitiza.

Aidha Nkumba alifafanua kuwa dhana ya kuichambua na kuikosoa Rasimu ya Mabadiliko ya Katiba  si kumdhalilisha Mwenyekiti wa Tume na Wajumbe wake. Hivyo msingi mzima wa kutolewa rasimu hiyo ni kwamba wananchi waichambue, kuikosoa, kuboresha, kuirekebisha na hata ikibidi kuibadilisha kabla ya kuipigia kura.

Alisema rasimu hiyo haikuletwa kama msahafu wala biblia na ndiyo maana zimewekwa hatua mbili  baada ya kazi ya tume kumalizika, ambazo ni bunge hilo na kura ya maoni ya wananchi. Aliwataka wajumbe wa bunge hilo kushirikiana ili kuweza kuifanya kazi hiyo. Wajumbe wa bunge hilo wa Tanzania Kwanza wapo takribani 400 na watatoka katika makundi mbalimbali, ambayo msimamo wao ni kushawishi kwa hoja na wala hawatalazimisha.