Na Ronald Ndungi, EANA, Arusha
JUMUIYA ya Afrika Mashariki (EAC) ina jumla ya wakazi zaidi ya milioni 20 wanaokabiliwa na umasikini sugu, watafiti wamebainisha mwishoni mwa wiki.
Mkurugenzi wa Kanda wa Taasisi ya Maendeleo Afrika (DIA), Charles Ntale aliwaambia waandishi wa habari mjini Nairobi, Kenya kwamba kama hakutakuwa na sera za makusudi za kupambana na umasikini, takwimu hizo zitaongezeka katika kipindi cha miaka 10 ijayo.
“EAC hainabudi kutoa msukumo katika kuimarisha mtangamano ili kuhakikisha kwamba maendeleo yanawafikia pia jamii zilizopo pembezoni,” alisema Ntale wakati wa uzinduzi wa Ripoti ya Umasikini Sugu ya 2014 hadi 2015.
Ripoti hiyo imeandaliwa na Taisisi ya Ushauri ya Umasikini Sugu inayofanyakazi katika nchi 15 zinazoendelea duniani. Umoja wa Mataifa(UN) umeweka lengo la kumaliza umasikini sugu ifikapo mwaka 2030.
Alisema nchi nyingi wanachama wa EAC zina sera ambazo zinadhaniwa kwamba maendeleo yatashuka hadi kuwafikia raia.
“Lakini kwa bahati mbaya hili halitokei kwa sababu ya muundo wa kiuchumi na kisiasa ulipo katika nchi hizo,” alisema.
Aliongeza kuwa kazi za Mashirika yasiyo ya Kiserikali (NGOs) ni ndogo mno kuweza kupunguza kiasi cha umasikini katika kanda hiyo.
“Ukweli ni kwamba ni kazi ya serikali kuhakikisha kwamba raia wake hawaishi katika dimbwi la umasikini,” alisema.
Alibainisha kwamba siasa na itikadi za kijamii zinakwamisha juhudi za kumaliza tatizo la umasikini katika kanda hiyo.