Na Joachim Mushi
RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania leo mjini Dodoma amelihutubia Bunge Maalum la Katiba na kulizinduwa rasmi, huku akionekana wazi wazi kupinga mfumo wa Serikali tatu uliopendekezwa na Tume ya Mabadiliko ya Katiba katika rasimu yake iliyowasilishwa kwa wabunge.
Akizungumza kwa hisia Rais Kikwete ameukosoa mfumo wa Serikali tatu kwa madai kuwa Serikali hiyo ya Tatu ambayo ni ya Muungano wa Tanzania itashindwa kufanya kazi zake kwa ufasaha kwa kuwa itakuwa haina vyanzo vya mapato vya uhakika na kutoseleza utekelezaji uendeshaji.
Alisema Serikali washirika yaani Tanganyika na Zanzibar ndizo zitakazokuwa na vyanzo vya mapato na rasilimali hivyo endapo upande mmoja wa washirika utagoma kuchangia fedha kwenye Serikali ya Muungano Serikali hiyo itakosa uwezo na kuanguka. Hata hivyo alionesha hofu endapo kutaibuka dola ya Tanganyika jambo ambalo litasababisha kuanza kwa mgawanyiko wa utaifa, kwani wananchi wataanza kuulizana na kufukuzana kwamba wa Tanzanyika wabaki Tanganyika na Wazanzibari warudi kwao.
“Dhana nyingine ambayo imependekezwa na tume na kuvuta hisia za wengi ni muundo wa Serikali yetu, kuwa wa Serikali tatu badala ya mbili za sasa pendekezo hili limezua mjadala mkubwa tangu lilivyotolewa katika rasimu ya kwanza na kurudiwa katika rasimu ya pili, wakati mwingine mjadala umekuwa mkali na hisia kali kwa kila upande kwa kweli hili ndilo jambo kubwa kuliko yote katika rasimu, na ndio kazi kubwa kuliko yote katika bunge hili…kila Mtanzania anasubiri kuona uamuzi wenu utakuwa upi…ombi langu kwenu kwanza muwe watulivu ondoeni jazba maana wenye hasira hawajengi,” alisema Kikwete.
“…Lakini mtambue uamuzi usiokuwa sahihi kwa jambo hili (Serikali tatu) unahasara kubwa, mnaweza kuingiza nchi yetu kwenye matatizo na kuwa na mazingira magumu, vurumai na nini…na yote tuliojenga kwa nusu karne yakapotea, Tanzania inaweza kuwa ni nchi iliyojaa migogoro yenye matatizo ambayo atujawai kuyapata…,” alisema Rais Kikwete.
Alisema suala la Serikali tatu si mara ya kwanza kupendekezwa lakini mara zote lilishindikana kupita. Aliwataka wabunge kulijadili kwa kina ili safari hii limalizike na kuondokana na hali ya kujitokeza mara kwa mara. “…Suala hili ilikuwa kiini cha kuchafuka kwa hali ya siasa mwaka 1984 Zanzibar…mi nafurahi kuwa jambo hili linazungumzwa sasa lizungumzeni kama linakubaliwa likubaliwe au kukataliwa likataliwe ili tufanye shughuli nyingine,” alisema Kikwete.
Aidha hoja nyingine zilizopo katika rasimu ambazo ameonesha wasiwasi ni uwepo ukomo wa kugombea ubunge, wananchi kuwa na mamlaka ya kumvua mbunge wao kabla ya kipindi cha uchaguzi na rasimu kukataza wabunge kuwa mawaziri. Akifafanua zaidi alisema wapo watu wanaweza kutumia vibaya uamuzi huo hivyo kuanzisha vitina na kujikuta wananchi wanampinga mbunge wao ili aondoke na kuhusu ukomo wa ubunge utawanyima watu fursa za kuwatumikia wananchi huku wakiwa na nguvu na nia ya ufanya hivyo.
Alisema mfumo wa mawaziri kuwa wabunge kwa maana nyingine unamfanya waziri kuhojiwa bungeni na kuulizwa maswali na wabunge kwa kuwa nayeye anaingia bungeni lakini endapo hawataingia bungeni huenda ikashindikana kuwabana kama ilivyo sasa kwa kuwa wao si sehemu ya wabunge.
Alisema wapo baadhi ya watu wamelalamika rasimu kuwa na mambo mengi jambo ambalo linaleta mkanganyiko na kuainisha baadhi ya mambo ambayo yanaweza kuigharimu Serikali na kujikuta ikishtakiwa kwa kile kutotekeleza mambo ambayo haina uwezo nayo. “…Rasimu imetaja mambo mengi; mbegu, mbolea, pembejeo, haki ya mtoto kupewa jina, lishe bora…tusipotekeleza haya tunaweza kujikuta tunalaumiwa kwa kutumia katiba na hata kupelekwa mahakamani,” alisema Rais Kikwete.
Aliwataka wajumbe hao kuisoma kwa umakini rasimu nzima kifungu kwa kifungu sura kwa sura ili kujiridhisha kabla ya kufanya uamuzi wa kupitisha. Alisema kazi ya tume imemalizika na kazi iliyopo ni kwa wajumbe hao kuandika katiba itakayokubaliwa na Watanzania wote na inayo waunganisha na kuwasaidia katika kuleta maendeleo kwa kila raia.
Alisema hata takwimu zilizotolewa na tume kwamba Wananchi wanaotaka Serikali tatu ni wengi na Serikali tatu haiepukiki zina ulakini hivyo kuwataka wajumbe wa bunge hilo kuhakikisha wanaleta katiba itakayo kubaliwa na wengi na si kukataliwa na wananchi kwenye kura za maoni hapo baadaye.
Mtandao huu (dev.kisakuzi.com) utachapisha hotuba nzima ya Rais aliyoitoa katika Bunge Maalumu kwa wasomaji wetu kupata fursa ya kuipitia.