Na Mwandishi Wetu
CHAMA Cha Mapinduzi (CCM) kimetoa kauli ikiwa ni siku mbili baada ya Mwenyekiti wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba nchini Jaji Joseph Sinde Warioba kuwasilisha kwenye Bunge maalum la Katiba rasimu ya pili ya katiba ambayo itajadiliwa na wajumbe.
Katika kauli yake ambayo imesainiwa na Katibu wa Halmashauri Kuu ya CCM, Itikadi na Uenezi, Nape Nnauye kwa vyombo vya habari leo imesisitiza kuwa msimamo wa chama hicho ni kuwa na Serikali mbili kama ilivyo sasa na kurekebisha baadhi ya changamoto zinazojitokeza katika mfumo huo.
Nnauye alisema tangu Jaji Warioba alipowasilisha rasimu ile bungeni juzi, kumekuwa na maombi mengi ya watu kutaka kujua msimamo wa CCM juu ya baadhi ya mambo hasa muundo wa muungano ambapo alisisitiza msimamo wa chama hicho bado ni uleule.
Alisema CCM ndio waasisi wa Muungano huu wa Tanganyika na Zanzibar hivyo, CCM inamasilahi makubwa na mapana na Muungano huo kama waasisi na pengine kuliko taasisi nyingi ndani na nje ya nchi yetu hivyo inakila sababu ya kuulinda.
“Bado CCM inaamini changamoto za Muungano huu suluhisho lake sio kubadili muundo wa Muungano bali ni kuufanyia maboresho muundo wa muungano tulionao wa serikali mbili. Hivyo basi CCM bado inaamini muundo bora kwasasa utakao dumisha muungano wetu ni muundo wa Serikali mbili,” alisema Nnauye.
“…Kwakuwa kazi ya Warioba na Tume yake sasa imekwisha rasmi, kuisha kwa kazi yao ni mwanzo wa awamu nyingine ya mchakato huu. Mwisho wa kazi ya Tume sio mwisho wa mjadala juu ya Katiba tuitakayo bali ni mwanzo wa awamu nyingine ya mjadala mpana na maboresho kama sio marekebisho ya kuondoa mapungufu kwenye rasimu iliyowasilishwa,” alisema.
Alisema hata hivyo mwanzo wa awamu hii nyingine ni fursa nzuri ya kupima kama kweli yaliyomo kwenye rasimu na maelezo ya ziada yaliyotolewa na Jaji Warioba yana akisi maoni ya Watanzania walio wengi.
“CCM ina amini awamu mbili zilizobaki kwakuwa zinahusisha wawakilishi wa wananchi kupitia Bunge maalum la Katiba, na hatimaye itawahusisha wananchi wenyewe moja kwa moja kupitia kura yao, zitatumika vizuri kutupa ni nini hasa matakwa ya Watanzania juu ya Katiba waitakayo na sio maoni au matakwa ya wachache,”
“Wakati haya yote yakiendelea CCM bado tunaamini Muungano huu ni muhimu ukadumishwa na kuimarishwa. CCM tunaaamini ili Muungano huu udumu njia pekee kwasasa ni kufanya marekebisho kwenye Muundo wa serikali mbili ili ujibu vizuri zaidi changamoto mbalimbali zilizoibuliwa na kukidhi mazingira ya sasa.”
Tunawaomba wanaCCM na watanzania kwa ujumla kuwa watulivu katika kipindi hiki. Ni vizuri Watanzania tukavumiliana, tukashindana kwa hoja tukitanguliza mbele uzalendo na masilahi ya kweli ya nchi yetu.