Jaji Warioba Awasilisha Rasimu kwa Bunge la Katiba Dodoma, Hotuba Yake Yasisimua…!

Jaji Joseph Warioba

Jaji Joseph Warioba

Na Joachim Mushi

MWENYEKITI wa Tume ya Katiba, Jaji Joseph Warioba leo amewasilisha Rasimu ya Katiba kwenye Bunge maalumu la Katiba, tendo ambalo limekwenda sambamba kwa kufafanua kwa kina mgawanyiko ibara na sura ya rasimu hiyo ambayo itajadiliwa na wajumbe hao wa katiba. Hotuba nzito aliyoitoa itoa imesisimua wabunge ikiwa ni pamoja na kukatishwa mara kadhaa kwa kelele za kuungwa mkono na baadhi ya wajumbe.

Tukio hilo limefanyika mjini Dodoma, ambapo Jaji Wariomba na Makamu Mwenyekiti wa Tume hiyo, Jaji Agustino Ramadhani waliingia ndani ya ukumbi wa Bunge Maalumu la Katiba na kuwasilisha rasimu ya Katiba katika bunge hilo. Akifafanua muktasari wa rasimu Jaji Warioba alisema rasimu hiyo ina jumla ya ibara 271 huku ikiwa na sura 17, tofauti na katiba ya sasa ambayo ina ibara 152 pekee.

Akiwasilisha rasimu hiyo huku akifafanua ibara zake kwa kina na mapendekezo ya Tume ya Katiba, Jaji Warioba aliwahakikishia wajumbe wa bunge la katiba masuala yote ya msingi ambayo wananchi wameyapendekeza na kuona inafaa yameingizwa katika rasimu hiyo hivyo ni kazi ya wajumbe wa bunge hilo kujadiliana na kutoka na muafaka utakaolisaidia taifa.

Kati ya masuala ambayo Jaji Warioba alifafanua zaidi katika hotuba yake ya zaidi ya saa nne ndani ya bunge hilo, ni suala la Muundo wa Serikali Tatu lililopendekezwa na wananchi wengi waliotoa maoni kwa tume na pia tume hiyo kuliridhia baada ya kulifanyia utafiti wa kina, kutafakari na kupitia taarifa mbalimbali za pande zote.

Alisem ongezeko la ibara kwa rasimu ya sasa ni kutokana na maoni mengi ya wananchi waliyoyatoa wakati tume hiyo ikizunguka maeneo mbalimbali kukusanya maoni ya wananchi wote Tanzania Bara na Visiwani.

Alisema kati ya maeneo ambayo tume yake ilipokea maoni mengi ni katika suala la haki za binadamu pamoja na serikali tatu. Kiujumla alisema wananchi wengi walionekana kulalamika juu ya muundo uliopo sasa wa Serikali na kwamba kila upande wa muungano unaona unaona unanyonywa na upande mwingine, hivyo wanashauri muundo wa Serikali tatu utapunguza malalamiko ambayo yanatolewa na pande zote.

Alitolea mfano kuwa katika maoni ambayo wananchi, taasisi za umma na binafsi ambazo ziliwasilisha kutoka bara zinaonesha kulalamikia mwenendo wa muungano ambapo Tanzania Bara inaonekana kutengwa na upande wa Tanzania visiwani kwa masuala mbalimbali ilhali wao hawatengwi.

Alisema Zanzibar kwa sasa ina katiba yake bendera na hata wimbo wake wa taifa tendo ambalo Tanzania Bara linalalamikiwa kwa kuwa wao hawana kitu kama hicho zaidi ya kutumia bendera, katiba na wimbo wa taifa wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Hata hivyo kwa upande wa Zanzibar nao wananchi na taasisi zimelalamikia kutengwa na Serikali ya Tanzania kwa kuwa ndiyo Serikali ya Muungano (kwa madai yao) hivyo kupendekeza kila upande huwe huru kwa masuala yake na uwepo upande mwingine wenye jukumu la kufanya kazi kwa maslahi ya pande zote bila mgongano.

“…Ukitafsiri mapendekezo ya pande zote unaona kabisa kuwa wengi wanapendekeza uwepo muundo wa Serikali tatu, na wanaamini muundo huo utamaliza mvutano uliopo kwa pande zote,” alisema Jaji Warioba.

Alisema katika rasimu hiyo pia imepunguza madaraka ya rais ili kuongeza ufanisi na utendaji kazi tofauti na ilivyo katika katiba ya sasa, ikiwa ni pamoja na kupendekeza mawaziri na spika wasitokane na wabunge. Alisema tume yake imejiridhisha na kila pendekezo lililotolewa na wananchi kabla ya kuliingiza kwenye rasimu ikiwa ni pamoja na kuwatoa hofu juu ya matokeo yoyote ya mapendekezo katika rasimu hiyo.

Akiwasilisha hotuba hiyo wajumbe wengi walionekana wakipaza sauti kila mapendekezo ya Serikali tatu yalipotolewa na Jaji Warioba jambo ambalo lilionesha kuunga mkono kwa baadhi yao juu ya pendekezo hilo.

Bunge limehairishwa hadi hapo siku ya Ijumaa, ambapo pamoja na shughuli nyingine siku hiyo Rais wa Tanzania, Jakaya Kikwete saa kumi za jioni atalihutubia Bunge pamoja na kulizinduwa tayari kwa kuanza shughuli zake za kupitia na kujadili rasimu iliyowasilishwa na Jaji Warioba pamoja na timu yake ya tume ya Katiba.