Frank Mvungi-Maelezo
IMEELEZWA kuwa Tanzania ni miongoni mwa wazalishaji wakubwa wa magadi soda yatakayoingizia taifa Shilingi Bilioni 480 kwa mwaka. Hayo yamesemwa na Meneja Uhusiano na Mawsiliano wa Shirika la Taifa la Maendeleo (NDC), Abel Ngapemba akizungumza kwenye mkutano na waandishi wa habari leo jijini Dar es Salaam.
Ngapemba alisema hatua hiyo inatokana na kugunduliwa kwa kwa kiasi kikubwa cha madini hayo katika Bonde la Engaruka Wilayani Monduli mkoani Arusha. Alizitaja faida za kugundulika kwa madini ya magadi soda kuwa ni ajira zaidi ya 500 na fedha za kigeni kutokana na mauzo ya madini hayo nje ya nchi.
Alisema kuwa viwanda vinavyotegemea magadi soda kama malighafi ya uzalishaji hali itakayochochea kukua kwa sekta ya viwanda hapa nchini. Ngapemba alibainisha kuwa madini ya magadi soda yanatumika viwandani katika utengenezaji wa bidhaa kama vioo, sabuni, dawa za meno, dawa za hosipitali, uoakaji mikate, kutengeneza karatasi, nguo, na usafishaji wa maji.
Alifafanua kuwa utafiti uliofanywa na wataalamu wazalendo kuanzia mwaka 2010 hadi 2013 na ulifanyika kwa awamu tatu yakwanza ikiwa ni uchunguzi wa awali na kutafuta maeneo ya kufanyia uchorongaji ili kubaini wingi na ubora wa magadi soda. Alisema kuwa kazi iliyofanywa na kampuni ya OC, ambapo awamu iliyofuata ni kuangalia njia ya uvunaji wa magadi soda hayo iliyofanywa na JSC Service.
“Matokeo ya utafiti huo yameonyesha kuwapo kwa magadi soda kiasi cha mita za ujazo bilioni 4.7 na inakadiriwa kila mwaka wastani wa mita za ujazo milioni 1.9 zinaongezeka katika eneo hilo,” alisema Ngapemba na kuongeza: Alisema kuwa NDC itahakikisha kuwa katika utekelezaji wa miradi hii mazingira hayataathiriwa na tunu za taifa zitalindwa ambapo mtazamo wa shirika hilo ni kuwapo kwa mradi wa uvunaji magadi, utalii, na ufugaji.