Na Mwandishi Wetu,
CHAMA Cha Mapinduzi (CCM) kimeibuka na ushindi wa kishindo baada ya kumshinda mpinzani wake mkuu Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) katika uchaguzi mdogo wa kugombea nafasi ya ubunge Jimbo la Kalenga, Mkoani Iringa. Kwa mujibu wa taarifa ambazo mtandao huu umezipata CCM imepata kura 22,962 ikiwa ni sawa na asilimia 79.32 huku Chama cha Chadema kikiambulia jumla ya kura 5,853 ikiwa ni sawa na asilimia 20.22.
Taarifa zaidi zinasema chama pekee cha upinzani kidogo kilichoshiriki uchaguzi huo CHAUSTA ambacho hadi muda wa kampeni unamalizika kilikuwa hakichafanya rasmi uzinduzi wa kampeni zake kimeambulia jumla ya kura 150 ikiwa ni sawa na asilimia 0.52 ya ushindi. Jumla ya wapiga kura wote waliojitokeza siku ya uchaguzi walikuwa 29,541 na kura zilizoharibika zilikuwa 576. Hata hivyo idadi ya wapiga kura ambao walijiandikisha walikuwa 71,964 katika jimbo zima.