Bondia Fadhili Awadhi Mwananyamala

Bondia Fadhili Awadhi

Bondia Fadhili Awadhi

BONDIA wa ngumi za kulipwa nchini Fadhili Awadhi amefariki dunia katika hospitali ya Mwananyamala baada ya kuugua kwa siku kadhaa. Fadhili Awadhi alikuwa ni miongoni mwa mabondia waliochaguliwa kucheza mpambano wa ubingwa Machi 29, 2014 dhidi ya mpinzani wake toka Mkoani Tanga, Alan Kamote.

Taarifa ambayo mtandao huu umeipata kutoka kwa kiongozi wa ngumi nchin, Ibrahim Kamwe zinasema sababu ya kifo chake kwa mujibu wa madaktari wa Mwananyamala imetokana na ugonjwa wa malaria, ambapo alitumia dozi ya metakelfin na hali ilibadilika pale alipojaribu kufanya  mazoezi na kujisikia vibaya.

Baada ya kujisikia vibaya mazoezini aliwahishwa katika hospitali hiyo ambayo alikaa kwa siku mbili akiendelea na matibabu na hatimaye umauti ulimkumba. “…Alikuwa katika maandalizi ya mpambano wake huo,” alisema Kamwe.

Fadhili Awadhi (32) alikuwa anaendelea vizuri katika mchezo huo kiasi cha kufikia kucheza pambano la ubingwa katika ukumbi wa PTA sabasaba, akiwasindikiza mabondia Japhet Kaseba na Thomas Mashali. Alisema shughuli za mazishi zinafanyika nyumbani kwao maeneo ya Manzese.

“…Sisi tulimpenda lakini mungu alimpenda zaidi…tunaomba ailaze roho ya marehemu Fadhili Awadhi ‘tiger’ peponi,” alisema.