KLABU ya Simba itafanya mkutano wa wanachama wake Jumapili (Machi 16 mwaka huu) kwa ajili ya kuifanyia marekebisho Katiba yao. Nachukua fursa hii kuwatakia kila la kheri katika mkutano huo ambao ni muhimu katika kuhakikisha klabu yao inapiga hatua katika maendeleo ya mpira wa miguu na ustawi wake kwa ujumla.
Hata hivyo, nawakumbusha viongozi na wanachama wa klabu ya Simba kuwa marekebisho hayo ni lazima yafanyike kwa kuzingatia Katiba, Kanuni na maelekezo ya Shirikisho la Kimataifa la Mpira wa Miguu (FIFA), Afrika (CAF) na Tanzania (TFF).
Aidha waraka wa TFF kwa wanachama wake wa Februari 7 mwaka huu uzingatiwe kikamilifu katika marekebisho hayo.
TFF inawatakia wanachama wa Simba mkutano mwema, na inawakumbusha wazingatie umuhimu wa kudumisha amani na maelewano katika klabu yao.
SEMINA YA WAAMUZI YAANZA DAR
Semina ya siku mbili kwa waamuzi wenye beji za Shirikisho la Kimataifa la Mpira wa Miguu (FIFA) na wale wa ngazi ya juu nchini (elite) kwa robo ya kwanza ya mwaka huu inaanza kesho (Machi 15 mwaka huu) kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Waamuzi na waamuzi wasaidizi 22 kutoka Tanzania Bara na Zanzibar wanashiriki katika semina hiyo ambayo pia itahusisha mtihani wa utimamu wa mwili (physical fitness test), na itamalizika keshokutwa (Machi 16 mwaka huu).
Baadhi ya waamuzi hao ni Charles Simon kutoka Dodoma, Dalila Jafari (Zanzibar), Ferdinand Chacha (Mwanza), Hamis Chang’walu (Dar es Salaam), Helen Mduma (Dar es Salaam), Israel Mujuni (Dar es Salaam), Issa Vuai (Zanzibar), Janeth Balama (Iringa) na Jesse Erasmo (Morogoro).
John Kanyenye (Mbeya), Jonesia Rukyaa (Bukoba), Josephat Bulali (Zanzibar), Lulu Mushi (Dar es Salaam), Martin Saanya (Morogoro), Mfaume Nassoro (Zanzibar), Mohamed Mkono (Tanga), Mwanahija Makame (Zanzibar), Ngaza Kinduli (Zanzibar), Ramadhan Ibada (Zanzibar) na Waziri Sheha (Zanzibar).
YANGA KUIVAA MTIBWA SUGAR VPL
Ligi Kuu ya Vodacom (VPL) inaendelea kesho (Machi 15 mwaka huu) kwa mechi tatu ambapo mabingwa watetezi Yanga wataumana na Mtibwa Sugar kwenye Uwanja wa Jamhuri mjini Morogoro.
Nao vinara wa ligi hiyo, Azam wanaikaribisha Coastal Union ya Tanga katika mechi itakayofanyika Uwanja wa Azam Complex uliopo Chamazi jijini Dar es Salaam.
Mechi nyingine itachezwa Uwanja wa Kaitaba mjini Bukoba kwa kuwakutanisha wenyeji Kagera Sugar dhidi ya maafande wa Tanzania Prisons kutoka jijini Mbeya.