Miradi ya BRN Yatumia Bilioni 500

Miradi ya BRN Yatumia Bilioni 500

Miradi ya BRN Yatumia Bilioni 500


Frank Mvungi – Maelezo

SERIKALI imetumia zaidi ya bilioni 500 katika utekeleaji wa miradi ya Matokeo Makubwa Sasa katika kipindi cha Julai hadi Desemba, 2013. Hayo yamesemwa na Kiongozi wa Miradi ya Matokeo Makubwa Sasa (BRN) wa Wizara ya fedha Bw. Emmanuel Tutuba wakati wa mkutano na waandishi wa habari.

Akieleza zaidi Bw. Emmanuel alisema Serikali imefanikiwa kutekeleza miradi mbalimbali chini ya mpango wa BRN ambapo alitaja miradi hiyo kuwa ni Elimu iliyopewa jumla ya shilingi bilioni 8.3 na miradi ya maji imepewa shilingi bilioni 86.
Alitaja miradi mingine kuwa ni ya kilimo ambayo imepewa jumla ya shilingi bilioni 10.2 na miradi ya uchukuzi iliyopewa shilingi bilioni 146.6.

Aidha Bw. Emmanuel alitaja miradi mingine kuwa ni ya nishati iliyopewa jumla ya shilingi bilioni 339.4 ili kusaidia katika kuimarisha Sekta ya nishati ili kusaidia. Emmanuel aliongeza katika kipindi cha Julai hadi Desemba, 2013 jumla ya shilingi bilioni 215 zimekusanywa kutokana na vyanzo vipya vya kodi vilivyoibuliwa na maabara ya matokeo makubwa sasa.

Jumla ya shilingi bilioni 10.9 zimekusanywa kutokana na utekelezaji wa hatua za kuongeza mapato yasiyo ya kodi kwa kutoa leseni za kuvuna mazao ya misitu na vitalu vya uwindaji wa kitalii kwa njia ya mnada.

Uboreshaji wa kukusanya kodi ya majengo na kodi ya ardhi katika Halmashauri za Manispaa za Temeke, Ilala, na Kinondoni unaendelea vizuri ikiwa ni moja ya chanzo kipya cha mapato ambapo halmashauri hizo zimetumika kama sehemu za majaribio kabla ya kuenezwa katika halmashauri zote nchini ili kuongeza mapato. Hata hivyo Serikali imeamua kuanzisha utekelezaji wa miradi ya ubia kati ya Sekta ya Umma na Sekta Binafsi yenye thamani ya shilingi trilioni 6 hadi kufikia mwaka 2015/16.

Miradi ya awali ambayo imebainishwa kuanza kutekelezwa kwa ubia ni ujenzi wa barabara ya Dar es Salaam hadi Chalinze, uendeshaji wa mradi wa mabasi yaendayo haraka jijini Dar es Salaam na ujenzi wa kituo cha kufua umeme cha Kinyerezi.
Naye Mwenyekiti wa mradi wa matokeo makubwa sasa toka Wizara hiyo Bi Alvera Ndabagoye alitoa wito kwa vyombo vya habari kuwaelimisha wananchi kuhusu miradi ya matokeo makubwa sasa ili kuongeza ushiriki wa wananchi katika kukuza uchumi.
Kauli ya Matokeo Makubwa Sasa (BRN) ni utaratibu unaotumiwa na Serikali katika kusimamia na kufuatilia utekelezaji wa vipaumbele katika Sekta sita zinazolenga kuongeza ukuaji wa uchumi ambazo ni Elimu, Maji, Nishati, Kilimo, Uchukuzi na Afya kwa kushirikisha wadau wote.