RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Jakaya Mrisho Kikwete asubuhi ya kesho, Ijumaa, Machi 14, atamwapisha Katibu wa Baraza la Wawakilishi, Yahya Khamis Hamad kuwa Katibu wa Bunge Maalum la Katiba. Aidha, katika sherehe fupi itakayofanyika Ikulu Ndogo, Dodoma, Rais Kikwete atamwapisha Katibu wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. Thomas Didimu Kashililah kuwa Naibu Katibu wa Bunge Maalum la Katiba.
Taarifa iliyotolewa jioni ya, Machi 13, mwaka huu wa 2014 mjini Dodoma na Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi Ombeni Y. Sefue inasema kuwa Rais Kikwete atawaapisha Katibu na Naibu Katibu wa Bunge Maalum la Katiba kwa mujibu wa kifungu cha 24(7) cha Sheria ya Mabadiliko ya Katiba, Sura ya 83, toleo la mwaka 2014.
Bwana Hamad na Dk. Kashilillah wanashika nafasi hizo kwa mujibu wa Kifungu cha 24(1) cha Sheria ya Mabadiliko ya Katiba, Sura ya 83, toleo la mwaka 2014, ambacho kinasema kuwa nafasi za Katibu na Naibu katibu wa Bunge Maalum la Katiba zitajazwa na Katibu wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Katibu wa Baraza la Wawakilishi, Zanzibar. Kwa mujibu wa kifungu cha 24(3) cha sheria hiyo, Sura ya 83, toleo la mwaka 2014, Katibu wa Bunge Maalum atatoka upande tofauti na ule anakotoka Mwenyekiti wa Bunge Maalum.
Kwa vile aliyechaguliwa kuwa Mwenyekiti wa Bunge Maalum, Samuel John Sita anatoka Tanzania Bara, basi Katibu wa Bunge anakuwa Bwana Yahya Khamis Hamad ambaye ni Katibu wa Baraza la Wawakilishi, Zanzibar na Naibu Katibu wa Bunge Maalum la Katiba anakuwa Dk. Kashililah ambaye ni Katibu wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.