RAIS Jakaya Mrisho Kikwete amemtumia salamu za rambirambi Muadhama Polycarp Kardinali Pengo na Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania (TEC) kufuatia kifo cha Mhashamu Askofu Mstaafu Fortunatus Lukanima aliyekuwa Askofu wa Jimbo Kuu Katoliki la Arusha.
“Kwa masikitiko makubwa napenda kutoa pole zangu za dhati kwa kuondokewa na kiongozi mahiri wa kidini katika jamii yetu” Rais amesema na kueleza kuwa si wakatoliki na familia yake tu ambao wameondokewa na mpendwa wao bali “Kwa pamoja tumepoteza kiongozi wetu wa kiroho, mshauri mkubwa mwenye mapenzi na watu wake na nchi kwa ujumla” Rais ameongeza.
“Naungana nanyi nyote katika kipindi hiki kigumu cha majonzi, Familia ya Marehemu na jamii yote ambayo Marehemu Baba Askofu alitumikia kwa moyo wake wote kwa upendo mkubwa. Hatuna namna ya kufarijiana bali kwa pamoja kuungana na kumuombea Marehemu Baba Askofu mapumziko mema ya Milele” Rais amesema.
Rais ametuma rambirambi hizo mara baada ya kupokea taarifa rasmi kutoka Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania (TEC) ambayo imemtaarifu kuhusu kifo hicho kilichotokewa tarehe 12 March katika Hospitali ya Rufaa ya Bugando ambapo Marehemu alikua akipata matibabu.
Marehemu anatarajiwa kufanyiwa ibada yake ya mazishi Jumamosi tarehe 15 March, Mungu ailaze roho ya Marehemu Askofu Mstaafu Lukanima mahali pema Peponi, Amina.