Sensa Yaonesha Idadi Kubwa ya Watanzania ni Watoto, JK Apokea Taarifa

Rais Jakaya Mrisho Kikwete akipokea toka kwa Kamishna wa Sensa Hajjat Amina Mrisho Ripoti ya Mgawanyo wa Watu kwa Umri na Jinsia kwa data za sensa ya watu na makazi mwaka 2012 leo Machi 13, 2014 Ikulu jijini Dar es Salaam. PICHA NA IKULU

Rais Jakaya Mrisho Kikwete akipokea toka kwa Kamishna wa Sensa Hajjat Amina Mrisho Ripoti ya Mgawanyo wa Watu kwa Umri na Jinsia kwa data za sensa ya watu na makazi mwaka 2012 leo Machi 13, 2014 Ikulu jijini Dar es Salaam. PICHA NA IKULU

Rais Jakaya Mrisho Kikwete akiwa na Kamishna wa Sensa Hajjat Amina Mrisho (kushoto) na Mkurugenzi Mkuu wa Ofisi ya Taifa ya Takwimu Dk. Albina Chuwa baada ya kupokea Ripoti ya Mgawanyo wa Watu kwa Umri na Jinsia kwa data za sensa ya watu na makazi mwaka 2012 Machi 13, 2014 Ikulu jijini Dar es salaam

Rais Jakaya Mrisho Kikwete akiwa na Kamishna wa Sensa Hajjat Amina Mrisho (kushoto) na Mkurugenzi Mkuu wa Ofisi ya Taifa ya Takwimu Dk. Albina Chuwa baada ya kupokea Ripoti ya Mgawanyo wa Watu kwa Umri na Jinsia kwa data za sensa ya watu na makazi mwaka 2012 Machi 13, 2014 Ikulu jijini Dar es salaam

Na Mwandishi Maalumu

PIRAMIDI ya Idadi ya Watu nchini Tanzania inaonesha kuwa idadi kubwa ya watu hapa nchini ni watoto wenye umri wa chini ya miaka 15 na vijana. Asilimia 44 ya watu wote hapa nchini ni watoto wenye umri chini ya miaka 15, ambapo utafiti wa Mama na Mtoto wa Mwaka 2010 unaonesha kuwa kiwango cha uzazi ni wastani wa watoto 5.4 kwa kila mama mwenye umri wa kuzaa ambao ni miaka 15-49.

Sera ya Vijana Tanzania ya Mwaka 2007 inatambua Vijana kuwa ni watu wote wenye umri wa miaka 15-35, ambapo kulingana na Sensa ya Mwaka 2012 ni asilimia 34.7 ya watu wote hapa nchini.

Mkurugenzi Mkuu wa Ofisi ya Taifa ya Takwimu Dk. Albina Chuwa amemueleza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete leo Ikulu wakati akimkabidhi vitabu na majedwali yenye matokeo na machapisho ya Sensa ya Watu na Makazi ya Mwaka 2012.

Kulingana na Takwimu, idadi ya watu Tanzania imeongezeka zaidi ya mara tatu kutoka watu Milioni 12.3 kwa Mwaka 1967 hadi watu milioni 44.9 Mwaka 2012. Takwimu hizo zinaonesha kuwa Mkoa wa Dar es Salaam una asilimia kubwa ya Vijana wenye umri wa miaka 15-35 wakati Mkoa wa Singida ukiwa na asilimia ndogo zaidi.

Kulingana na Takwimu, zaidi ya nusu ambayo ni asilimia 52.2 ya watu wote nchini, wako katika umri wa kufanya kazi ambapo Mkoa wa Dar es Salaam unaongoza kwa kuwa na asilimia kubwa ya watu wenye umri huu wa kufanya kazi na Mkoa wa Simiyu uko chini zaidi kwa kuwa na asilimia 45.5 ya watu hawa.

Katika takwimu hizo, zaidi ya nusu ya watu katika Mikoa ya Simiyu, Rukwa na Geita ni Watoto wenye umri wa chini ya miaka 15. Dk. Chuwa pia amebainisha kuwa Takwimu zinaonesha kuwa rasilimali watu kwa ajili ya kuzalisha na kuongeza Uchumi na kupunguza Umaskini sio tatizo hapa nchini na kinachotakiwa ni watu wote kutumia fursa zilizopo nchini kufanya kazi kwa bidii na maarifa ili kuinua uchumi wa Nchi.

Kulingana na takwimu asilimia 5.6 ya watu hapa nchini ni wazee na takwimu hizi zinaonesha kuwa wazee kwa asilimia kubwa wako katika Mikoa ya Kilimanjaro, Mtwara, Lindi na Pwani ambapo asilimia ndogo zaidi wapo katika Mikoa ya Dar es Salaam na Mjini Magharibi. Kwa mujibu wa Sera ya wazee Tanzania, Mzee ni mtu mwenye umri wa miaka 60 au zaidi.

Takwimu pia zinazidi kuonesha kuwa asilimia ya watu wanaoishi Mijini imeongezeka zaidi ya mara tano ambapo ni asilimia 6.4 mwaka 1967 na kufikia asilimia 29.6 kwa mwaka 2012. Jiji la Dar es Salaam lina asilimia 10 ya watu wote hapa Tanzania Bara wakati Mjini Magharibi ina asilimia 46 ya watu wote wa Zanzibar. Sensa pia imeonesha kuwa Wanawake ni wengi zaidi , kwa asilimia 51 ukilinganisha na wanaume ambao ni asilimia 49 kama ilivyo katika nchi nyingi Barani Afrika.

Hapa Tanzania Mkoa wa Manyara unaongoza kwa kuwa na idadi kubwa ya Wanaume ambapo Mkoa wa Njombe una idadi ndogo zaidi ya wanaume.