Na Mwandishi Wetu
MJUMBE wa Bunge Maalumu la Katiba na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano), Bi. Samia Suluhu Hassan amechaguliwa leo mjini Dodoma kuwa Makamu Mwenyekiti wa Bunge Maalumu la Katiba.
Bi. Samia Suluhu amechaguliwa jioni hii mjini Dodoma kwa jumla ya kura 390 ikiwa ni sawa na asilimia 74.6 baada ya kumshinda mgombea mwenzake waliokuwa wakichuana naye, Bi. Amina Abdallah Amour aliyejipatia kura 12 sawa na asilimia 24.1. Katika uchaguzi huo jumla ya wajumbe waliopiga kura ni 523 na kura 7 ziriharibika ikiwa ni sawa na asilimia 1.3.
Bi. Samia ambaye ni Mbunge wa Jimbo la Makunduchi mjini Zanzibar alionekana kuungwa mkono na idadi kubwa ya wajumbe wa bunge la katiba hasa wanawake tangu jana alipojitokeza kuchukua fomu kwani aliambatana na idadi kubwa ya wajumbe wanaomuunga mkono jambo ambalo lilionesha neema kwa upande wake tofauti na mpinzani wake Bi. Amina Amour.
Bi. Samia sasa anaungana na Mwenyekiti wa Bunge hilo, Samuel Sitta aliyechaguliwa jana kuongoza bunge hilo maalumu ambalo linatarajiwa kuanza kazi zake mara moja baada ya zoezi la kuwaapisha wabunge hao kufanywa na bunge kuzinduliwa rasmi.