Sugu apigwa ‘stop’ Mbeya

Joseph Mbilinyi ‘Mr Sugu’.


MBUNGE kijana kutoka Jimbo la Mbeya kwa tiketi ya Chama Cha Demokrasia na Maendeleo, (CHADEMA), Joseph Mbilinyi ‘Mr Sugu’ amepigwa marufuku na Jeshi la Polisi kufanya mikutano ya hadhara kutokana na sababu zilizotajwa kuwa ni za kiitelejensia.

Taarifa zilizopatikana kutoka Mbeya zinasema kuwa, Sugu alizuiliwa na polisi kufanya mikutano ndipo alilazimika kuwasiliana na viongozi wake wa kitaifa jijini Dar es Salaam ambao waliamua kuchukua hatua ya kuzungumza na Waandishi wa habari juzi Jumapili kuzungumzia tukio hilo na mengine yanayofanana na hilo.

Wanasheria waandamizi wa Chadema, Mabere Marando na Mkurugenzi wa Sheria, Katiba na Haki za Binadamu wa chama hicho, Tundu Lisu walilazimika kufanya mkutano na Waandishi wa habari kuelezea madai yao jinsi gani jeshi la polisi haliwatendei haki ya kikatiba wabunge wao.

Lisu alisema kuwa chama chake kilikuwa kimejipanga vizuri kwa wabunge wake kufanya mikutano ya hadhara ikiwa ni njia moja wapo ya kutoa shukrani kwa wananchi waliowachagua wabunge na madiwani wa chama chake kwa wingi msimu huu kuliko vipindi vingine vyote, tangu mfumo wa vyama vingi uanze mwaka 1992.

Ameongeza kusema kuwa karibu kila mikoa waliyokuwa wamejipanga wamezuiliwa kufanya mikutano hali inayowanyima haki wabunge kuzungumza na wapiga kura wao na akasitiza kuwa kitendo hicho ni shambulio la waziwazi kwa haki, kinga na mamlaka ya Bunge ambazo zinatambulika kimataifa na zinalindwa na katiba na sheria ya kinga ya Mamlaka na haki za Bunge 1988.

Aliahidi kuwa Chadema itafanya kila linalowezekana kuhakikisha kwamba haki za wabunge wao kuzungumza na wananchi zinalindwa kwa kutumia Mamlaka na Haki za Bunge ili waweze kufanya kazi waliyotumwa na wapiga kura wao bungeni ili kuwasilisha hoja na mambo ya msingi ya wananchi.