Danny Mwakiteleko, kulia akiwa mjini Arusha hivi karibuni akihudhuria Mkutano Mkuu wa Wahariri Tanzania, kushoto ni baadhi ya wahariri wenzake kutoka vyombo mbalimbali vya habari.
NAIBU Mhariri Mtendaji wa New Habari (2006), Danny Mwakiteleko amefariki dunia usiku wa kuamkia leo. Mwakiteleko ambaye hivi karibuni alipata ajali mbaya eneo la TIOT, kuelekea Tabata jijini Dar es Salaam, akitokea kazini amefariki baada ya kulazwa kwa muda katika Hospitali ya Rufaa Muhimbili tangua apate ajali.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Katibu Mkuu wa Jukwaa la Wahariri nchini (TEF), Nevilli Meena, zinasema; mwanahabari huyo mkongwe amefariki ikiwa ni siku chache tangu apate ajali baada ya kugongana na lori majira ya saa nne usiku eneo la TIOT, gari ambalo lilitoweka mara baada ya kufanya ajali hiyo.
“Danny alikuwa amelazwa MOI kwa matibabu baada ya kupata ajali siku mbili, tatu zilizopita katika eneo la TIOT Tabata alipokuwa akitoka kazini kurejea nyumbani usiku.”
“Ni msiba mkubwa kwetu wana habari kwa kumpoteza Mhariri mwenzetu. Pole kwa familia ya Danny, pole kwa wafanyakazi wa New Habari, pole kwa wahariri wote wa Tanzania, pamoja na ndugu, jamaa na marafiki wote wa Danny ambao kwa namna moja au nyingine wameguswa na msiba huu. Bwana alitoa na bwana ametwaa jina lake lihimidiwe,” alisema Meena.