UMOJA wa Mataifa (UN) umesisitiza mataifa yote ulimwenguni kuhakikisha yanafuata usawa wa kijinsia kwa wanawake na wasichana na si tu kwa sababu ni suala la haki za msingi za binadamu, lakini kwa sababu maendeleo katika maeneo mengine mengi yanategemea suala hilo. Ujumbe huu unaoenda sambamba na maadhimisho ya Siku ya Wanawake Duniani umetolewa na taasisi hiyo ya kimataifa katika ujumbe wake maalumu kwa vyombo vya habari kuelekea kwenye sherehe za maadhimisho ya siku hiyo.
“… Siku ya Wanawake Duniani, tunasisitiza umuhimu wa usawa wa kijinsia kwa wanawake na wasichana sio tu kwa sababu ni suala la haki na haki za msingi za binadamu, lakini kwa sababu maendeleo katika maeneo mengine mengi yanategemea hili,” ilisema taarifa hiyo ya UN.
Taarifa hiyo imesema nchi ambazo kuna usawa zaidi wa kijinsia zimekuwa na ukuaji mzuri wa kiuchumi, huku makampuni ambayo yana viongozi wengi wanawake nayo yanafanya vizuri. Imefafanua kuwa pamoja na hayo makubaliano ya amani ambayo yanahusisha wanawake yamekuwa yakidumu kwa muda mrefu zaidi ukilinganisha na kwingineko.
“..Mabunge yenye wanawake wengi hutunga sheria nyingi zaidi juu ya masuala muhimu ya kijamii kama vile afya, elimu, kupambana na ubaguzi na msaada wa watoto. Ushahidi uko wazi: usawa kwa wanawake ni maendeleo kwa wote. Suala la ukweli ni muhimu tunapofanya kazi kuharakisha maendeleo kuelekea kwenye Malengo ya Maendeleo ya Milenia kwa tarehe ya mwisho ya mwaka ujao na kutengeneza ajenda kwa miaka inayofuata ya baada ya 2015,” ilieleza taarifa hiyo.
Hata hivyo taarifa hiyo imefafanua kuwa mafanikio muhimu yamepatikana katika upatikanaji wa elimu ya msingi kwa ajili ya wasichana na uwakilishi wa kisiasa na wanawake. Lakini mafanikio bado ni madogo na yanatofautiana.
“…Msichana anayezaliwa leo bado anakabiliwa na kukosekana kwa usawa na ubaguzi, bila kujali mama yake anaishi wapi. Tuna wajibu wa kuhakikisha anapata haki yake ya kuishi mazingira yasiyo vurugu ambayo huathiri mwanamke mmoja katika wanawake watatu duniani; haki ya kupata mshahara sawa na kwa kazi sawa; kuwa huru na ubaguzi unaozuia haki yake ya kushiriki katika uchumi; kuwa na haki ya usawa katika kusemea maamuzi yanayoathiri maisha yake; haki ya kuamua kama anataka na lini atakuwa na watoto, na ni wangapi.”
“Mimi nina ujumbe kwa kila msichana aliyezaliwa leo, na kwa kila mwanamke na msichana aliye juu ya sayari: kutambua haki za binadamu na usawa si ndoto, ni wajibu wa serikali, Umoja wa Mataifa na kila binadamu. Mimi pia nina ujumbe kwa ajili ya wanaume wenzangu na wavulana: timiza wajibu wako. Sisi sote tunafaidika wakati wanawake na wasichana – mama yako, dada, marafiki na wafanyakazi wenzako – wanapewa nafasi ya kufikia uwezo wao.”
“Kwa pamoja, basi, tufanye kazi kufikia haki za wanawake, uwezeshaji na usawa wa kijinsia wakati tukijitahidi kuondoa umaskini na kukuza maendeleo endelevu. Usawa kwa wanawake ni maendeleo kwa wote!” ilisema taarifa hiyo ya UN.