RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. Jakaya Kikwete amemtumia Salamu za Rambirambi Mufti wa Tanzania, Sheikh Shaaban Bin Simba kufuatia kifo cha Sheikh wa Mkoa wa Iringa, Alhaj Sheikh Ally Juma Tagalile (96) kilichotokea usiku wa kuamkia tarehe 6 Machi, 2014 katika Hospitali ya Mkoa wa Iringa alikokuwa amelazwa akisumbuliwa na ugonjwa wa shinikizo la damu.
“Nimeshtushwa, nimesikitishwa na kuhuzunishwa sana kutokana na taarifa za kifo cha Sheikh wa Mkoa wa Iringa, Alhaj Sheikh Ally Juma Tagalile kilichotokea usiku wa kuamkia tarehe 6 Machi, 2014 katika Hospitali ya Mkoa wa Iringa alikokuwa amelazwa kwa matibabu akisumbuliwa na ugonjwa wa shinikizo la damu”, amesema Rais Kikwete katika Salamu zake.
Rais Kikwete amesema kifo cha Alhaj Sheikh Ally Juma Tagalile ni pigo kubwa siyo tu kwa Waumini wa Dini ya Kiislamu Mkoani Iringa ambao hakika walikuwa wanamtegemea sana kiuongozi katika masuala ya kiroho, bali pia kwa Waumini wa Dini hiyo kote nchini.
“Natambua kuwa enzi za uhai wake, Marehemu Alhaj Sheikh Ally Juma Tagalile pia alitoa mchango mkubwa katika Utumishi wa Umma hususan katika Sekta ya Afya akiwa na Taaluma ya Udaktari, hivyo kuondoka kwake kumetunyang’nya kama Taifa uzoefu wake mkubwa katika Taaluma ya Afya”, ameongeza kusema Rais Kikwete katika kuomboleza kifo chake.
“Kutokana na msiba huo mkubwa, ninakutumia wewe Mufti wa Tanzania, Sheikh Shaaban Bin Simba Salamu zangu za Rambirambi na pole nyingi kwa kumpoteza mmoja wa Viongozi wa ngazi ya juu wa Dini ya Kiislamu hapa nchini. Ninamuomba Mwenyezi Mungu, Mwingi wa Rehema aipokee na kuilaza Mahala Pema Peponi Roho ya Marehemu, Alhaj Sheikh Ally Juma Tagalile, Amina”, amezidi kusema Rais Kikwete katika kuomboleza kifo cha Marehemu..
Rais Kikwete amemuomba Mufti Sheikh Shaaban Bin Simba kumfikishia Salamu zake za Rambirambi na pole nyingi kwa familia ya Marehemu Alhaj Sheikh Ally Juma Tagalile kwa kupotelewa na Kiongozi na Mhimili muhimu wa familia. Amewaomba wawe na moyo uvumilivu na ujasiri ili wahimili machungu ya kuondokewa na mpendwa wao kwa kutambua kuwa yote ni Mapenzi yake Mola.
Aidha Rais Kikwete ameihakikishia familia ya Marehemu kuwa yuko pamoja nao katika kipindi chote cha kuomboleza kifo cha mpendwa wao kwani msiba huu ni wa wote.