Serikali Makete Yatoa Bati kwa Waathirika wa Maafa ya Kimbunga

Mkuu wa Wilaya ya Makete, Josephine Matiro akiwa na waathirika wa kimbunga katika Kijiji cha Ndulamo, Makete alipokuwa akiwakabidhi misaada ya mabati.

Mkuu wa Wilaya ya Makete, Josephine Matiro akiwa na waathirika wa kimbunga katika Kijiji cha Ndulamo, Makete alipokuwa akiwakabidhi misaada ya mabati.

Baadhi ya sehena ya mabati yaliyotolewa na serikali kwa waathirika wa kimbunga.

Baadhi ya sehena ya mabati yaliyotolewa na serikali kwa waathirika wa kimbunga.

Mkuu wa wilaya ya Makete, Josephine Matiro akizungumza na waathirika wa kimbunga katika ofisi za Kijiji cha Ndulamo.

Mkuu wa wilaya ya Makete, Josephine Matiro akizungumza na waathirika wa kimbunga katika ofisi za Kijiji cha Ndulamo.

Na Edwin Moshi, Makete

HALMASHAURI ya Wilaya ya Makete kwa kushirikiana na mfuko wa jimbo, umekabidhi msaada wa mabatia 180 kwa waathirika wa maafa ya kikumba kilichoezua nyumba 10 katika Kijiji cha Ndulamo wilayani Makete ikiwa ni ahadi ya Serikali kwa waathirika hao.

Akizungumza na waathirika wa tukio hilo wakati wa kukabidhi bati hizo zenye thamani ya sh. milioni 2.5, Mkuu wa Wilaya ya Makete, Josephine Matiro alisema kufuatia mkutano uliofanyika baina ya serikali na wananchi wa kijiji hicho, waligawana majukumu ambapo serikali iliahidi kutoa bati kwa wananchi hao.

Matiro alisema ingawa msaada huo haukuwa asilimia 100 kwa waathirika wote lakini wamepatiwa zaidi ya robo tatu hivyo kiasi kilichobakia ni kidogo na kuwaomba wananchi hao kumalizia gharama zilizobaki ili kumaliza janga hilo.

“Mfano mtu alikuwa ameharibikiwa nyumba yenye bati 24, hapa serikali inampa bati 20 na hizo nne anatakiwa azigharamie mwenyewe, na hii ni kutokana na msaada huo kuhitajika katika vijiji vingine viwili vya Makete ambavyo vilikumbwa na maafa tena ili kila mmoja apate kidogo kidogo,” alisema Matiro.

Aliongeza kuwa hivi sasa hawana budi pia kumshukuru Mbunge wa Jimbo la Makete ambaye pia ni Waziri wa Mazingira, Dk. Binilith Mahenge kwa jitihada zake na uongozi wa wilaya kwa ujumla kuhakikisha wananchi hao wanapata bati hizo na kuwaomba kuzitumia kwa makusudi yaliyopangwa na si kuziuza.

Awali akimkaribisha Mkuu wa wilaya, Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Makete, Peter Mwagilo alisema ilifanyika tahmini ya kina na wataalamu wa halmashauri mara baada ya maafa hayo kuwakumba wananchi na hivyo kila mwananchi atapewa bati kulingana na ukubwa wa tatizo lake.

“Kwa mfano wapo waliopata maafa kidogo wanahitaji bati chache, wengine bati mbili hao watapata zote mbili, lakini wale waliopata maafa makubwa watapata bati nyingi ila kila mmoja atagharamia kiasi kidogo pale palipopelea,” alisema Kaimu Mkurugenzi.

Naye mmoja wa waathirika hao akizungumza na mwandishi baada ya kukabidhiwa bati zake, Bi. Ami Mahenge alisema anaishukuru serikali kwa msaada huo aliopewa na kuongeza kuwa kutokana na maafa hayo yaliyomkumba hakujua hatima ya maisha yake, ukizingatia yeye kutokuwa na uwezo wa kifedha lakini msaada huo umekuwa mkombozi wa maisha yake.

Bi. Mahenge ametoa wito kwa waathirika wenzake kuhakikisha wanatumia ipasavyo msaada huo, kwa kuwa kumekuwa na kasumba ya kutumia vibaya misaada na baadaye wanaishia kulalamika.