Na Mwandishi Wetu
KATIBU wa Idara ya Uhamasishaji na Chipukizi wa jumuiya ya Umoja wa Vijana wa Chama Cha Mapinduzi (UVCCM) ambaye pia ni Mjumbe wa Bunge Maalum la katiba Ndugu Paul Makonda amefanya ziara ya kikazi katika Mkoa wa Singida na kusimika makamanda wateule wa jumuiya ya Vijana wa Kata 16 za wilaya ya Singida Mjini.
Shughuli hiyo ya kusimika makamanda 16 iliyofanyika Katika Mkutano wa hadhara katika uwanja wa Ukombozi uliopo Kata ya Majengo Singida Mjini ilihudhuriwa na mamia ya wananchi ambao walijitokeza kumsikiliza kiongozi huyo wa Jumuiya ya Vijana.
Akiongea na wananchi, Paul Makonda amewataka Makamanda hao wateule kufanya kazi kwa ajili ya Jumuiya, Chama na wananchi, amewataka watambue kuwa nafasi hiyo ni kubwa na ya msingi kwa Maendeleo ya Vijana na wananchi kwa Ujumla.
Lakini pia amewataka wananchi wa Singida na watanzania wa mikoa yote kujitambulisha kimikoa katika sura ya kimataifa kwa aina ya zao wanalozalisha, aliwataka wanasingida kujitambulisha kwa zao la alizet na kutumia kilimo kama nyenzo muhimu ya kijiletea Maendeleo ya Kiuchumi.
Katika mkutano huo, Makonda alikabidhi kadi kwa vijana Zaidi ya 50 ambao waliamua kujiunga na Jumuiya ya Umoja wa Vijana wa Chama Cha Mapinduzi na kupokea wanachama wengine kutoka Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) wakiongozwa na kiongozi wa Vijana wa CHADEMA wa Kata hiyo ndugu Yasin Athuman.
Pia, aliwananga Viongozi wa Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) kuacha za Ukanjanja za kutumia matatizo ya wananchi kama daraja la kufikia mafanikio yao binafsi. Asema wanashindwa kutumia rasilimali zao kujiimarisha kama Chama na kusaidia kutatua matatizo ya wananchi badala ya kutumia fedha nyingi kwa kukodi helkopta na kufanya matumizi yasiyo na msingi yasiyojali mustakabal mwema wa Wananchi.
Pia amsifu na kumpongeza Tundu Lissu kuwa ni kiongozi mjanja ndani ya Chama hicho kwani baada ya kugundua kuwa Chama hicho kinaendeshwa kiukoo na kifamilia nae akamchukua Dada yake anayeitwa Christina Lissu na kumpa Ubunge wa Viti maalum.