RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Jakaya Mrisho Kikwete anatarajia kulizinduwa bunge maalumu la Katiba wiki ijayo mjini Dodoma. Awali Rais Kikwete alitarajia kulizinduwa bunge hilo, Februari 28, 2014 kabla ya ratiba ya bunge hilo kubadilika.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa hivi karibuni na Kurugenzi ya Mawasiliano ya Ikulu; imesema hata hivyo rais hatokuwa na hotuba yake ya mwisho wa mwezi (Februari) kama ilivyo kawaida.
“Hotuba hiyo haitakuwepo kwa sababu awali Rais Kikwete alitarajiwa kuzindua Bunge Maalum la Katiba kwa hotuba rasmi Bungeni mjini Dodoma kabla ya ratiba ya shughuli za Bunge hili kufanyiwa mabadiliko. Rais Kikwete sasa atalizindua Bunge hilo wiki ijayo,” ilibainisha sehemu ya taarifa hiyo. Hata hivyo taarifa hiyo haikutaja siku mahususi ya uzinduzi.
Bunge maalumu la Katiba linaloendelea mjini Dodoma bado linaendelea kujadili rasimu ya kanuni ambazo zitaliendesha bunge hilo kabla ya kuanza vikao vyake rasmi baada ya taratibu za awali kukamilika.