• Adai ni mzigo, anawadanganya na kuwapotosha wananchi
• Asisitiza ni sehemu ya tatizo la mgawo wa umeme
• Asema si mgeni serikalini, ni mchochezi, mnafiki na mfitini
• Aonya anaigawa, anaitumbukiza CCM kwenye shimo
• Asema mambo yakiendelea hicho mwaka 2015 CCM itaambulia patupu
MWENYEKITI wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Dar es Salaam, John Guninita amemlaumu Waziri wa Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Samwel Sitta akidai ni mnafiki na mchochezi anayetumika kuigawa CCM na kukitumbukiza chama hicho kwenye shimo.
“Sitta ni sehemu ya serikali na si mgeni serikalini. Alikuwapo tangu kipindi cha Mwalimu Nyerere, na pia alikuwa Spika wa Bunge. Kwa nafasi hizi yeye ni sehemu ya tatizo na siyo kuwadanganya wananchi na kuwapotosha kwa kuirushia serikali lawama.
‘Anaudanganya umma. Anataka kujenga umaarufu ambao siyo wa kwake. Kama ni kuharibu waliharibu wote na siyo kusema tatizo ni la serikali.
‘Sitta amekuwa mchawi wa CCM… chama kinajimaliza chenyewe tena kwa kutumia viongozi wa nafasi za juu.,” alisema Guninita.
Guninita alikuwa akizungumza katika mkutano wa hadhara Mbezi na Mbezi kwa Msigani katika jana, katika ziara ya kutekeleza agizo la Mwenyekiti wa CCM, Rais Kikwete la kuleta mageuzi ndani ya chama hicho na ‘kujivua gamba’.
Alisema hali ya siasa ndani ya chama hicho si shwari kutokana na mgawanyiko mkubwa wa baadhi ya viongozi ambao wanazungumza wanavyojisikia bila kujali maslahi na ukweli ndani ya Chama hicho.
“Kilichotufikisha hapa tulipo leo ni unafiki na fitina za viongozi kama Sitta ambao hawaeleweki wanafanya nini ndani ya chama chetu. Ndiyo maana viongozi wanajiuzulu ovyo, kitu ambacho siyo sahihi, chama kinapoteza makada muhimu na kuwaacha watu mizigo na wafitini.
“Namshangaa Waziri Sitta, ana uwezo wa kwenda kwa Rais muda anaojisikia na pia alikuwa na nafasi ya kuyasema mambo yale katika vikao vya chana “party caucus”, na pia kwenye vikao vya Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) lakini anaropoka mambo kama hayo mbele ya umma wa watanzania na kuwapa umaarufu wapinzani.
“Amekosa busara kwa kuwa amekiuka maagizo ya Rais. Tunajua hakutumwa na Rais, bali alikurupuka tu, na bila kujijua anaiponda Ilani ya Uchaguzi ya CCM ambayo ndiyo muongozo wa kutekeleza majukumu yetu.
‘Mawaziri na wabunge wanasema tofauti na Rais anavyosema kuhusu matatizo ya umeme kwa sasa,” alisema Guninita
Alisema kauli mbovu za baadhi ya viongozi ambazo hazina ukweli zinabomoa chama, na kama CCM haitakauwa makini na kuwaonya wapotoshaji hao katika uchaguzi mkuu wa 2015 chama hicho kitaambulia patupu.
“Upinzani wanajipanga vizuri katika kuhakikisha mwaka 2015 wanachukua nchi, na kwa hali hii tulio nayo … kwa kauli za akina Sitta watafanikiwa kwa kuwa chama kitakuwa kimeyumba na kukosa imani kwa wapigakura wake.
“Haya siyo maneno ya Waziri, huyu jamaa ana mambo yake anayotekeleza… haiwezekani Sitta leo kuyasema haya, labda ana hasira za kukosa Uspika wakati yalikuwa makubaliano ya CCM kumuondoa kwa mafanikio ya chama na kutimiza sera ya 50 kwa 50.
‘Nilimsikia akisema kuwa atatembea mikoa yote kulisema hilo, lakini nawahakikishia kuwa hatafika Dar es Salaam labda aje na barua ya Mwenyekiti au Katibu Mkuu wa CCM kuwa wamemruhusu kupotosha jamii. Nasema kuwa hatutakubaliana na uongo wake,” alisisitiza Guninita.
Hivi karibuni, katika mkutano wa hadharani mjini Mbeya, Sitta pamoja na mambo mengine, alikaririwa akishauri serikali iwaombe radhi wananchi kutokana na tatizo la mgawo wa umeme unaoendelea nchini hivi sasa.
Guninita alisema mkutano wa jana ni matunda ya makubaliano ya kujivua gamba kama alivyoagiza Mwenyekiti Kikwete na kuwataka viongozi wote wa CCM kutembelea matawi na mashina katika maeneo yao kuyajua matatizo ya wapiga kura wao na kuimarisha mizizi ya chama ambayo ipo katika mashina na matawi.