WAFADHILI wameanza kufunga ushirikiano wa kuipa msaada nchi ya Uganda baada ya Rais Yoweri Museveni kutia saini muswada wa taifa hilo kupinga mapenzi ya jinsia moja wiki iliyopita.
Tangu tamko la nchi hiyo kupinga mapenzi ya jinsia moja katika vyombo vya habari tayari nchi tatu za Ulaya zimeamua kukata misaada yao kwa nchi ya Uganda kiasi ambacho ni mamilioni ya dola.
Nchi ya Uganda hutegemea asilimia 20 ya bajeti kutoka kwenye michango ya wafadhili yakiwemo mataifa ya kimagharibi. Wizara ya fedha ya Uganda ilisema inasubiri mawasiliano rasmi ya nchi husika, na iko tayari kukabiliana na athari za hatua hiyo.
Hadi kufikia sasa Waziri wa Fedha Wa Sweden, akiwa mjini Kampala, alisema wawekezaji kutoka nchi yake watakuwa na wakati mgumu kuweka pesa zao nchini Uganda kwa sababu watakuwa na hofu kuwa sheria iliopitishwa na taifa la Uganda inawadhulumu watu (wawekezaji).
Jana serikali ya Uholanzi ilisema itazuia kwa muda misaada kwa Serikali ya Uganda. Norway na Denmark pia zimetangaza kupunguza au kusimamisha kwa muda misaada yake kwa Uganda.
-BBC