Na Eleuteri Mangi- Maelezo, Mtwara
SERIKALI imeahidi kuangalia uwezekano wa kuwafadhili wanafunzi wapatao 20 kutoka mikoa ya Lindi na Mtwara wanaosoma katika chuo kikuu kishiriki cha Stella Maris Mtwara (STEMUCO) ambao hawana uwezo wa kulipa ada ya masomo yao.
Kauli hiyo imetolewa na Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini Eliakim Maswi alipokuwa akijibu ombi lililotolewa na Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha STEMUCO, Padre Dk. Aidan Msafiri alipokuwa akiwasilisha mada yake ya Tunu na maadili katika rasilimali za gesi, mafuta na madini kwa amani na maendeleo ya Tanzania wakati wa siku ya pili ya kongamano la viongozi wa dini kutoka mikoa ya Lindi na Mtwara. Katibu Mkuu Maswi alisema kuwa serikali ipo tayari kuhakikisha inawapatia elimu hiyo ili waweze kihudumia jamii ya wanaLindi na Mtwara katika kujiletea maendeleo yao wenyewe na taifa kwa ujumla.
Lengo kubwa la kongamano hili lilikuwa ni kutoa elimu zaidi kwa viongozi wa dini kuhusiana na rasilimali za gesi asilia, mafuta na madini kwa ajili ya maendeleo ya nchi nzima kwa ujumla. Elimu hiyo ililenga kuwaelimisha viongozi hao wa dini ambao wanaushawishi mkubwa kwa waumini wanaowaongoza ambapo mada mbalimbali zilitolewa ili kuwajengea uwezo wa kuwaelimisha waumini wao juu ya masuala ya gesi asilia, mafuta na madini.
Mada zilizowasilishwa katika kongamano hilo ili kufanikisha uelewa wa pamoja kwa viongozi wa dini ni pamoja na Mtazamo wa Kitheolojia/Kidini juu ya rasilimali za gesi asilia, mafuta na madini iliwasilishwa na Sheikh Abubakar Zuberi, Maelezo ya jumla ya Wizara ya Nishati na Madini kuhusu za gesi asilia, mafuta na madini iliwasilishwa na Katibu Mkuu wa wizara hiyo Eliakim Maswi, Tunu na maadili katika za gesi asilia, mafuta na madini iliwasilishwa na Padre Dkt. Aidan Msafiri, Ushuhuda wa mwakilishi aliyehudhuria mafunzou ushirikishaji mang’amuzi ya uchumi wa gesi nchini Thailand iliwasilishwa na Hssan Gobbosi.
Mada nyingine ni Mipango ya matumizi ya gesi asilia katika mikoa ya Lindi na Mtwara iliwasilishwa na Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC) Yona Killagane, Uzoefu wa ushiriki wa wazawa katika masuala ya gesi asilia iliwasilishwa na Sultan A. Sultan na Maelezo ya Wizara yaliyowasilishwa na Mwara Shoo na Ally Samaje.
Aidha, Serikali kupitia Wizara ya Nishati na Madini imeridhia kuendelea kuwapeleka vijana wa mikoa hiyo kusoma VETA kwa muda wa miaka mitatu ili waweze kutumia fursa ya kugunduliwa kwa rasilimali mbalimbali katika mikoa hiyo. Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa TPDC Yona Killagane akiwasilisha mada juu ya mipango ya matumizi ya gesi asilia Lindi na Mtwara alisema kuwa zipo faida nyingi za mradi wa gesi kwa wananchi.
Killagane alizitaja faida hizo kuwa ni kujenga shule za chekechea, wanafunzi wanapata udhamini wa kusomeshwa shule za sekondari, kujengewa hospitali, kuwapatia maji safi, ajira na kupata umeme unaotokana na gesi aktika maeneo yao.
Kongamano hili la siku mbili la viongozi wa dini wa mikoa ya Lindi na Mtwara liliandaliwa na viongozi wa dini wa mikoa hiyo ikiwa ni muendelezo wa kongamano la kitaifa la viongozi hao lililofanyika mwezi Januari mwaka huu jijijni Dar es salaam.
Makonamano haya yote mawili yaliongozwa na kauli mbiu ya “Rasilimali zetu za gesi asilia, mafuta na madini kwa amanina maendeleo ya Tanzania.