Na Magreth Kinabo- Maelezo, Dodoma
KAMATI ya Kumshauri Mwenyekiti wa muda wa Bunge Maalum kuhusu Kanuni za Bunge maalum imewasilisha taarifa katika semina iliyoandaliwa kwa wajumbe wa bunge hilo, ambapo imependekezwa mambo mbalimbali, likiwemo kuwepo kwa Siwa na wagombea uenyekiti na makamu mwenyekiti kutojitoa katika nafasi zao baada ya uteuzi wa wagombea.
Akiwasilisha taarifa hiyo Mwenyekiti wa kamati hiyo, Profesa Costa Mahalu wakati wa semina hiyo kwa wabunge hao, alisema kuwepo kwa Siwa mahsusi ambayo baada ya bunge hilo kukamilisha shughuli zake litatunzwa kama kielelezo cha kumbukumbu ya tukio hilo muhimu la kihistoria.
Alisema Siwa hilo litakuwa na urefu wa mita 1.2, uzito wa 4.5kgs, madini ya dhahabu na aluminium na muonekano wenye alama mbalimbali, ambazo ni kitabu, michoro ya watu wa makundi mbalimbali walioshiriki kutunga Katiba ya Tanzania kwa mujibu wa sheria, rangi, nembo, bendera ya taifa na kalamu inaounganisha kichwa na mkonga.
Profesa Mahalu aliongeza kuwa kamati hiyo imependekeza kuwepo kwa Siwa mbili ili moja iwekwe kama kumbukumbu kwa upande wa Tanzania Bara na nyingine Zanzibar. Alisema kamati hiyo imeongeza kanuni za uchaguzi wa Mwenyekiti na Makamu Mwenyekiti wa Bunge Maalum, ambapo imeweka fomu ya mgombea wa nafasi hizo na karatasi ya kupiga kura.
Mambo mengine yaliyopendekezwa katika rasimu hiyo ni watu wenye mahitaji maalum kuruhusiwa kutumia vifaa maalum ili waweze kuonekana kwa urahisi kwa Mwenyekiti wa Bunge Maalum na kupewa nafasi ya kusema wakiwa katika ukumbi wa mikutano ya bunge hilo na wasaidizi wa wajumbe wenye mahitaji maalum waruhusiwe kuingia katika ukumbi huo ili wawasaidie wajumbe hao katika zoezi la kupiga kura na kupata usaidizi mwingine watakao uhitaji ukumbini.
Aidha alisema kamati hiyo imependekeza wakati Mwenyekiti wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba anapowasilisha Rasimu ya Katiba wajumbe wasiruhusiwe kuomba ufafanuzi, utaratibu au mwongozo wa Mwenyekiti.
Aliongeza kuwa kamati hiyo imependekeza katika uendeshaji wa shughuli za Bunge Maalum pale ambapo mjumbe hataridhika na uamuzi wa Mwenyekiti wa Bunge Maalum kuhusu sula linalohusu Kanuni za Bunge Maalum, mjumbe huyo atakata rufaa kwa Kamati ya Kanuni na Haki za Bunge, ambayo Mwenyekiti anayekatiwa rufaa hatakalia kiti, na pia rufani hiyo ifanyiwe kazi na taarifa yake itolewe katika bunge hilo ndani ya kipindi kisichozidi siku tano.
Pia imependekeza ili vikao wa bunge hilo vianze idadi ya wajumbe wa bunge hilo iwe nusu kwa nusu kutoka Tanzania Bara na Zanzibar, ambapo awali ilikuwa ni nusu ya wajumbe wote. Katika taarifa hiyo imependekezwa kuwa viongozi wa bunge hilo kwa kufuata misingi ya haki na bila upendeleo wowote wasiruhusiwe kuhudhuria vikao vyovyote ambavyo vinajadili na kuweka msimamo juu ya suala lolote linalojadiliwa au litakalojadiliwa na bunge hilo.
Profesa Mahalu alisema kamati hiyo inapendekeza kanuni mpya inayohusu Rais wa Jamhuri ya Muungano, Rais wa Zanzibar au Rais wa nchi nyingine kutambuliwa kama wageni rasmi wanaoweza kualikwa na Mwenyekiti wa bunge hilo na kulihutubia. Aidha alifafanua kwamba kamati hiyo inapendekeza kuainisha mavazi rasmi yanayoruhusiwa katika bunge hilo.