Mkuu wa Chuo UDSM Afariki Dunia, Rais Kikwete Aomboleza

Mkuu wa Chuo Kikuu cha Dar Es salaam (UDSM), Balozi Fulgence Kazaura

Mkuu wa Chuo Kikuu cha Dar Es salaam (UDSM), Balozi Fulgence Kazaura

RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Jakaya Kikwete ameeleza mshituko na masikitiko yake kufuatia kifo cha Mkuu wa Chuo Kikuu cha Dar Es salaam (UDSM), Balozi Fulgence Kazaura kilichotokea nchini India usiku wa jana, Jumamosi, Februari 22, 2014.

Katika salamu zake za rambirambi kwa Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Mheshimiwa Dkt. Shukuru Kawambwa, Rais Kikwete amesema: “Nimepokea kwa mshituko, masikitiko na huzuni taarifa ya kifo cha Mkuu wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Balozi Flugence Kazaura, ambacho nimejulishwa kuwa kimetokea katika Kituo cha Matibabu ya Kansa katika mji wa Chennai, nchini India.”

“Kwa hakika, kifo cha Mzee Kazaura siyo kwamba kimekipokonya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam kiongozi hodari na mwenye visheni kubwa, lakini kifo hicho kimeondolea Tanzania mmoja wa watumishi hodari wa umma. Mzee Kazaura pia alikuwa mtumishi mwaminifu na mwadilifu kwa nchi yake na sote tunaendelea kwa kumkumbuka kwa sifa hizo na mchango wake mkubwa katika utumishi wa umma,” amesema Rais Kikwete na kuongeza:

“Alithibitisha sifa hizo katika nafasi zote alizozishikilia katika maisha yake tokea alipokuwa Katibu Mkuu katika wizara mbali, hadi alipokuwa Balozi wa Tanzania Makao Makuu ya Umoja wa Ulaya (EU) na nchini Ubelgiji, hadi alipoteuliwa Mshauri Maalum wa Uchumi wa Rais, hadi alipokuwa Naibu Katibu Mkuu wa Jumuia ya Afrika Mashairiki (EAC) katika uongozi mbali mbali za Bodi za mashirika ya umma na binafsi na hata kwenye nafasi yake ya Ukuu wa Chuo Kikuu cha Dar Es salaam kwa miaka tisa. Tutaendelea kumkumbuka.”

Ameongeza Rais Kikwete: “Nakutumia wewe Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Dkt. Shukuru Kawambwa salamu zangu za rambirambi kufuatia msiba huu mkubwa. Aidha, kupitia kwako naitumia jumuia nzima ya Chuo Kikuu cha Dar Es Salaam pole nyingi kwa kuondokewa na kiongozi wao.”

“Nakuomba pia unifikisshie salamu zangu za pole nyingi kwa familia ya Mzee Kazaura. Wajulishe kuwa naungana nao katika kuomboleza kifo cha Mzee wetu huyu na kwamba msiba wao ni msiba wangu pia. Pia naomba wajue kuwa naungana nao katika kumwomba Mwenyezi Mungu, Mwingi wa Rehema, aiweke mahali pema peponi roho ya Marehemu Fulgence Kazaura. Amina.”