MTANDAO wa Jinsia Tanzania (TGNP) upepinga vikali matakwa ya wajumbe wa Bunge maalum la Katiba lililoanza Februari 18, 2014, kudai nyongeza ya posho kutoka shilingi 300,000/= hadi sh. 500,000/= kwa siku. Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Kaimu Mkurugenzi wa TGNP, Lilian Liundi jana kwa vyombo vya habari, imeelezea kusikitishwa na kitendo cha wawakilishi hao waliotumwa na wananchi Dodoma kujadili rasimu ya Katiba mpya kuelekeza akili na mawazo yao yote kwe posho badala kufanya kwanza kazi iliyowapeleka.
“Sisi TGNP Mtandao kama shirika linalotetea haki na usawa wa kijinsia katika kuhakikisha rasilimali za taifa zinawanufaisha wananchi wote hatukubaliani kwa namna yoyote na madai hayo ya wajumbe kudai posho zaidi kwa wakati huu ambao taifa lina uhaba mkubwa wa fedha na deni la taifa likiongezeka kwa kasi kubwa hadi kufikia trilioni 27,” alisema Liundi katika taarifa hiyo
Alisema TGNP inashangazwa na wabunge hao kukataa kiasi cha posho cha shilingi 300,000 kwa siku ilhali kuna baadhi ya watumishi serikalini na sekta binafsi wanalipwa chini ya kiasi hicho kama mshahara wa mwezi mmoja na kuendelea kupambana kulea familia kwa mshahara huo huo.
Alisema wabunge hao wanaokataa kulipwa shilingi 300,000 kama posho kwa siku moja ndiyo ambao wameshidwa kupigania haki za wanawake na wanaume wanaopata kima cha chini cha mishahara kipandishwe na kukidhi mahitaji yao.
“TGNP Mtandao tunapinga mpango huu wa kuongeza posho kwasababu unajenga tabaka miongoni mwa jamii na ndani ya Bunge na kuiingizia serikali mzigo wa gharama ambazo mwishowe atazilipa mwananchi masikini. Pia suala la posho tunaliona kama mbinu inayotumiwa na wanaisasa wachache wasio na uzalendo kutaka kuvuruga mchakato wa katiba mpya kwa kuhamisha mijadala yenye tija katika kuandika katiba mpya,” alisema Liundi katika taarifa hiyo.
Aidha Kaimu Mkurugenzi huyo amewataka wanasiasa kuheshimu mchakato huu ambao unatumia gharama kubwa za fedha za walipa kodi na kuhakikisha wananchi wanapata katiba mpya inayobeba masuala na sauti zao.
“Kamati iliyoundwa kufuatilia posho isipoteze muda kujadili suala hilo jambo ambalo litasababisha kuongezwa kwa muda wa Bunge hili zaidi ya siku 70. Tunatoa rai kwa wajumbe wote wa Bunge hili kuwa makini na kauli zao na kufanya kazi waliotumwa Dodoma kwa maslahi ya taifa na anayeona kwamba fedha hazimtoshi anapaswa kurudi nyumbani ili kutoa nafasi kwa wazalendo wa Taifa hili kuandika katiba ya Tanzania,” alisema.
Bi. Liundi akifafanua zaidi aliongeza kuwa wajumbe wanaovuruga mchakato huu wanapaswa kuchukuliwa hatua za kisheria kwa kuliingizia taifa hasara.