Waliofuata Posho Bunge la Katiba Bora Warudi Nyumbani…!

Wajumbe wa Bunge la Katiba wakiwa bungeni mjini Dodoma.

Wajumbe wa Bunge la Katiba wakiwa bungeni mjini Dodoma.


KIMSINGI inakera sana unapomuona mtu mzima na mwenye busara anafanya vitendo vya hovyo. Hiki ndicho kinachofanyika sasa kwa baadhi ya wajumbe wa bunge maalumu la Katiba Mjini Dodoma. Wanalalamika posho ya shilingi 300,000 kwa siku wanayopewa haiwatoshi hivyo wanataka walipwe zaidi ya kiasi hicho.

Narudia tena haya ni madai ya hovyo wadao dai wabunge hawa ambao baadhi ya watu na makundi yalianza kuwabatiza jina la Wazalendo. Baadhi ya makundi na taasisi ziliwabatizwa wazalendo kwa mtanzamo wa kuwa, watumie uzalendo wao na busara kuhakikisha taifa linapata Katiba nzuri inayomfaa kila Mtanzania.

Ikiwa hata kabla ya kuanza kazi maalumu ambayo wajumbe hawa wameteuliwa kuyawakilisha makundi mbalimbali ya jamii bungeni, tayari wameanza kulilia posho kwa manufaa ya matumbo yao na si taifa. Wanalalamika posho ya shilingi 300,000 kwa siku haiwatoshi hivyo wanataka waongezewe na kupata zaidi ya kiasi hicho kwa simu. Huu ni upuuzi.

Binafsi naamini wanaolilia posho kuongezwa si wajumbe wa dhati wa Bunge la Katiba. Bali ni mamluki ambao wameingia katika nafasi hizo bahati mbaya hivyo nia yao ni kuvuma fedha zaidi kuliko kazi walioenda kuifanya. Nasema ni mamluki kwa kuwa kama wameweka maslahi ya matumbo yao mbele zaidi ya kazi walioenda kuifanya Dododoma, kundi hili linaweza kununulika.

Nasema kununulika maana hadi sasa kuna makundi ambayo yamegawanyika katika wajumbe wa Bunge maalumu la Katiba na misimamo yao. Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) lazima kina msimamo wake katika kuchambua rasimu ya Katiba Mpya. Vile vile Chama Cha Mapinduzi (CCM) kina mtazamo na msimamo wake katika uchambuzi wa rasimu ya Katiba Mpya.

Yapo mambo ambayo CCM kama chama wanaamini yakipitishwa katika rasimu itakayojadiliwa na bunge hilo maalumu kwao mambo yataenda vizuri zaidi kiutawala. Hali hii ni vivyo hivyo kwa vyama kama CUF, NCCR-Mageuzi na vyama vingine vinavyotambulika nchini. Katika hali ya kawaida vyama hivi havishindwi kutumia ushawishi wa namna yoyote ili kuhakikisha misimamo yao na maoni yao yanaungwa mkono ili waweze kufanikisha hoja zao.

Wanaweza kutumia ushawishi wowote, ama kwa ukarimu na hata kwa kujipendekeza kwa wajumbe ambao tayari wameonesha njaa hasa wanaodai posho zaidi. Sasa cha kujiuliza wajumbe hawa wanashindwa kununuliwa na vyama? Jibu ni rahisi sana, wajumbe hawa wanaweza kulalia upande wowote wenye maslahi kwao na si taifa kama tulivyofikiri awali. Wananunulika kwa kuwa tayari wameonesha kuwa lengo lao hapo Dodoma si kujadili Rasimu ya Katiba Mpya bali ni kuganga njaa.

Kiasi cha shilingi 300,000 ambacho wabunge hawa wanakikataa ni mshahara wa mfanyakazi kwa mwezi. Na mtu huyu anaishi na familia yake na majukumu kemkem, lakini anavumilia. Naamini hata baadhi ya wajumbe wanaopigania wao kulipwa zaidi ya shilingi 300,000 wanajua kuwa wapo baadhi ya wafanyakazi Serikalini wanalipwa shilingi 300,000 kwa mwezi na kwa hali ngumu ya maisha wanaendelea kuganga njaa.

Leo hii badala ya kutengeneza mazingira mazuri ili kila mmoja anufaike na keki ya Taifa hili wao wameanza kuchumia matumbo yao. Ndio maana nalazimika kusema kwamba wajumbe hawa ni ‘mamluki’ na wameingia bahati mbaya kuwawakilisha Watanzania katika mjadala wa rasimu ya Katiba.

Hivi ni kweli kwamba wajumbe hawa wanamatumizi ya zaidi ya shilingi laki tatu kwa siku! Na ni kweli kwamba wanalipwa posho ya zaidi ya lakini tatu wanaosafiri ndani ya nchi kikazi (kwa wale wafanyakazi)! Kwa muda wa siku 70 za kukaa Dodoma kila mmoja wa wajumbe atalipwa shilingi milioni 21 (21,000,000) kama posho pekee. Je, ni kweli kwamba kiasi hiki hakiwatosi
kiuhalisia!

Kimsingi naungana na maoni ya baadhi ya viongozi wa vyama vya siasa na wachambuzi wa masuala ya siasa waliozungumza wakisema kama kuna mjumbe anaona hawezi kufanya kazi ya kuwakilisha kundi lake kwa shilingi 300,000 kwa siku afunge virago na kurejea nyumbani kwake ili wazalendo wengine wajaze nafasi yake na kazi iendelee. Katibu Mkuu wa CHADEMA, Wilbroad Slaa, Mwenyekiti Msaidizi wa Chama cha Wananchi, CUF, Julias Mtatiro kwa nyakati tofauti wamenukuliwa wakiwashauri wajumbe wasiotaka kufanya kazi hiyo kwa shilingi 300,000 kwa siku waondoke na kuwaachia wengine. Wapo pia wachambuzi wa masuala ya siasa wamezikika wakiunga mkono hoja ya viongozi hawa.

Namaliza kwa kushauri kwamba mjumbe yeyote ambaye anaoona kiasi cha shilingi 300,000 kwa siku hakimtoshi ajitoe na kuwaachia wenzake. Kwani wanachokidai hakina tofauti na ufisadi tunaoupigia kelele kila uchao. Najua tayari Mwenyekiti wa Muda wa Bunge la Katiba, Amir Pandu Kificho ameunda jopo linaloenda kuzungumza na Serikali juu ya kilio cha posho na huenda wakafanikiwa. Kilio cha Watanzania wanaopinga ufisadi huo utawarudia.

Mwandishi; Joachim Mushi wa www.thehabari.com
0756469470, mushi@dev.kisakuzi.com