Wabunge Bunge la Katiba Walalamikia Posho ya Shs 300,000, Wadai Haiwatoshi..!

Sehemu ya Ukumbi Maalumu wa Bunge la Katiba uliopo Mjini Dodoma.

Sehemu ya Ukumbi Maalumu wa Bunge la Katiba uliopo Mjini Dodoma.


Na Magreth Kinabo – Maelezo Dodoma

MWENYEKITI wa muda wa Bunge Maalum la Katiba, Ameir Pandu Kificho, ametangaza timu ya wajumbe sita kwa ajili ya kujadili kuhusu malalamiko ya posho ya sh. 300,000 yaliyotolewa na baadhi ya wajumbe wa Bunge Maalum la Katiba kuwa kiasi cha posho hiyo hakitoshi kuweza kuifanya kazi hiyo kwa umakini.

Kificho alitangaza majina hayo leo mjini Dodoma kabla ya kuanza kwa semina kwa wajumbe wa Bunge la Katiba mjini Dodoma kuhusu Sheria ya Mabadiliko ya Bunge la Katiba Sura ya 83 toleo la mwaka 2014.

“Kuhusu suala la kumudu kuishi vizuri na hii kazi nzito tuliyonayo bado halina majibu kwa sasa,” alisema Mwenyekiti huyo.
Huku Bunge hilo maalumu la Katiba likijiandaa kuanza vikao vyake tayari baadhi ya wajumbe wameanza kulalamikia kiasi cha sh. 300,000 wanachopewa wajumbe hao kwa siku kuwa hakitoshi, hivyo kuanza mchakato wa kuishinikiza Serikali iongeze posho.

Baada ya malalamiko hayo kuibuka, Mwenyekiti wa muda alilazimika kuunda timu ya kufuatilia suala hilo. Majina ya wajumbe watakao jadili malalamiko hayo ya posho ni pamoja na William Lukuvi, Mohammed Aboud Mohammed, Freeman Mbowe, Paul Kimiti, Asha Bakari Makame na Jenista Mhagama.

Alisema timu hiyo itakutana mara baada ya semina hiyo na ikiongozwa na Mwenyekiti huyo wa muda ili kuweza kukaa pamoja na kupanga namna ya kuweza kuiomba Serikali kuangalia jambo hilo na kuweza kupata majibu. Timu hiyo imeundwa baada ya baadhi ya wajumbe wa bunge hilo kulalamikia posho hizo ndani na nje ya ukumbi wa Bunge jana kuwa ni kidogo.

Hata hivyo, Katibu Mkuu wa Chadema Dk. Wilbrod Slaa amepinga malalamiko hayo akizungumza na Mwananchi na kudai posho ya Sh 300,000 kwa siku inatosha kabisa. “kwa kuwa hata wafanyakazi wengine wa serikali wanapokea mshahara wa laki tatu mwisho wa mwezi.” Alisema.

Mwenyekiti Msaidizi wa CUF, Julius Mtatiro anaunga mkono mtazamo huu. Katika waraka wa wazi aliouweka kwenye ukurasa wake wa Facebook, Mtatiro anaandika: “Shilingi laki tatu tunazopewa kwa siku zinatosha kabisa, ambaye hazimtoshi aongeze za kwake (ama) aondoke Dodoma ili kupisha wanaoweza kutunga katiba kwa posho ya Sh 300,000 waendelee.”