Na Mwandishi Wetu
MABONDIA Thomas Mashali na Japhet Kaseba wamesaini makubaliano ya kucheza pambano la ubingwa wa mabara ‘Universal Boxing Organization (UBO)’ pambano litakalopigwa Machi 29, 2014 katika Ukumbi wa Karume ndani ya viwanja vya maonesho ya Sabasaba jijini Dar es Salaam (PTA).
Pambano hilo linaandaliwa na Mratibu mashuhuri katika masuala ya ngumi za kulipwa nchini kutoka Mkoa wa Tanga, Ally Mwanzoa aliyeonesha kufurahishwa kwa nidhamu iliyooneshwa na mabondia hao wakati wa zoezi la kusaini mkataba wa makubaliano hayo yaliyofanyika katika Ukumbi wa vijana Kinondoni hafla iliyo shuhudiwa na viongozi wa ngumi na waandishi wa habari.
Akizungumza na waandishi wa habari kiongozi wa ngumi za kulipwa nchini, Ibrahim Kamwe aliyefatana na Anthony Ruta alisema makubaliano yamekwenda vizuri na wote wametia saini kupigana pambano hilo litakalopigwa katika uzani wa kilogram 79 na wamechukua malipo yao ya awali kuashiria kuwa pambano hilo lipo na kila mmoja amejigamba kumchakaza mwenzake siku hiyo na kujitengenezea mazingira mazuri katika ubingwa wake huo.