TV, Mito ya Makochi Yamfunga Jela Miaka 30 na Viboko 12

Televisheni

Televisheni


Yohane Gervas, Rombo
   
MAHAKAMA ya Hakimu Mkazi ya Wilaya ya Rombo imemhukumu Hilas Bahath (31) kwenda jela miaka 30 baada ya kupatikana na hatia ya wizi wa kutumia silaha. Awali mwendesha mashtaka wa Polisi, Mkaguzi, Bernad Machibya alidai mahakamani hapo kuwa mnamo mwaka 2008 huko tarafa ya Mkuu mshtakiwa akiwa na wenzake wawili walivamia, kuvunja na kuiba vitu mbalimbali vya ndani ikiwemo Runinga na mito ya makochi mali ya Anna Samweli.

Akisoma hukumu hiyo Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Wilaya ya Rombo, Naomi Mwerinde alisema kuwa baada ya kusikiliza kwa makini ushahidi uliotolewa na upande wa mashtaka ameridhishwa pasipo na shaka, hivyo amemtia hatiani mshtakiwa kwa kosa la wizi wa kutumia silaha.

Alisema katika maelezo yaliyotolewa kwa uthibitisho na upande wa mashtaka yanaonesha kuwa mshtakiwa anajihusisha na vitendo vya wizi na amekuwa tishio katika Wilaya ya Rombo jambo ambalo limewafanya wakazi wa wilaya hiyo kuishi kwa wasiwasi kwa kumhofia. Hivyo Hakimu Mwerinde alisema mshtakiwa amepewa adhabu hiyo pamoja na kuchapwa viboko kumi na mbili ili iwe fundisho kwake na kwa watu wengine ambao wanatabia kama hizo.

Aidha Katika hatua nyingine mshtakiwa ameongezewa hukumu ya mwaka mmoja kwa kosa la kutoroka mahakamani wakati kesi yake ilipokuwa ikisikilizwa ambapo aliruka ukuta wa mahakama na kutoroka kusikojulikana tangia mwaka 2010 na polisi waliendelea na juhudi za kumsaka na kufanikiwa kumkata Februari mwaka huu. Wakati mshtakiwa akisomewa hukumu hiyo alionekana kucheka na hadi hakimu alipomaliza kumsomea hukumu bado aliendelea kucheka hali iliyowafanya watu waliokuwa wamehudhuria katika mahakama hiyo nao kuangua vicheko.