Amir Pandu Kificho Achaguliwa Mwenyekiti wa Muda Bunge la Katiba

Amir Pandu Kificho

Amir Pandu Kificho


SPIKA wa Baraza la Wawakilishi la Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ), Amir Pandu Kificho amechaguliwa kuwa Mwenyekiti wa muda wa Bunge Maalumu la Katiba muda huu. Pandu Kificho amechaguliwa muda jioni hii mjini Dodoma baada ya kuwashinda wagombea wenzake wawili akiwemo Profesa Costaric Mahalu.

Uchaguzi huo ambao awali ulilazimika kurudiwa baada ya idadi ya wabunge waliopiga kura kutofautiana na idadi ya kura, ulimpa ushindi Kificho baada ya kuibuka na kura 393 huku akiwazidi wenzake, Magdalena Lubangula na Prof. Mahalu waliopata kura 84 kila mmoja.

Akizungumza mara baada ya kuchaguliwa Mwenyekiti huyo wa muda aliwashukuru wabunge wa Bunge la Katiba kwa kuonesha imani juu yake na kumchagua aweze kuwaongoza kwa muda. Kwa uchaguzi huo Kificho anapewa jukumu la kusimamia bunge hilo maalumu katika kupitisha kanuni zitakazo waongoza katika mijadala mbalimbali.

Akitoa taarifa baada ya kuchaguliwa, Kificho alisema kesho Jumatano kitafanyika kikao ambapo wabunge watapewa rasimu ya kanuni zitakazoongoza bunge la Katiba na wabunge wote wa bunge maalumu watagawiwa rasimu ya kanuni za kuendesha bunge la Katiba.

“Tarehe 20 kikao cha kazi kitaendelea kwa mjadala kuhusu rasimu ya kanuni hizo na Jumatatu Februari 24 rasimu itapitishwa.” Alisema.