Bunge Maalumu la Katiba Mpya Kuanza Leo Dodoma…!

Bunge Maalumu la Katiba Mpya Kuanza Leo Dodoma

Bunge Maalumu la Katiba Mpya Kuanza Leo Dodoma


Na Mwandishi Wetu,

MBUNGE maalumu la Katiba linaanza leo mjini Dodoma ikiwa ni safari mpya ya taifa kuelekea kupata Katiba Mpya itakayo ridhiwa na Watanzania wote. Jumla ya wabunge 639 wanatarajiwa kushiriki katika mjadala huo wa kuchambua maoni ya Rasimu ya pili iliyowasilishwa serikalimi na wajumbe wa kukusanya maoni kutoka kwa wananchi mwaka jana (2013).

Idadi ya wabunge hao maalumu wa bunge la Katiba inajumuisha wabunge wa bunge la Tanzania, wajumbe wa baraza la wawakilishi Zanzibar na Wajumbe maalumu wawakilishi walioteuliwa na rais wa Tanzania kutoka katika makundi mbalimbali ya jamii.

Makundi yaliotoa wawakilishi ni pamoja na kutoka taasisi zisizokuwa za kiserikali, taasisi za kidini, vyama vya siasa vyenye usajili wa kudumu, taasisi za elimu, watu wenye ulemavu , vyama vya wafanyakazi, vyama vinavyowakilisha wafugaji, vyama vinavyowakilisha wavuvi, vyama vya wakulima na vikundi vya watu wenye malengo yanayofanana.

Akizungumza jana na waandishi wa habari Katibu wa Bunge, Dk. Thomas Kashililah alisema bunge hilo litaanza kwa wajumbe kupewa mwongozo na kuchangua mwenyekiti wa muda atakayeongoza vikao kuelekea kuwapata viongozi maalumu wa Bunge la Katiba.

Viongozi ambao watatakiwa kuchanguliwa baada ya kuchukua fomu na kuomba nafasi ni pamoja na Mwenyekiti wa Bunge la Katiba na Msaidizi wake na Katibu. Bunge hilo litafanya vikao vyake kwa siku 70 za awali na endapo halita maliza shughuli zake litalazimika kuongeza siku zingine 20, kumalizia kazi. Bunge hilo linatarajia kuanza rasmi majira ya saa nane mchana baada ya wabunge kukutana asubuhi na kupewa taratibu anuai ikiwemo ya matumizi ya ukumbi huo maalumu wa Bunge la Katiba.

Hata hivyo wakati bunge hilo likianza tayari makundi mbalimbali yameanza kuonesha msimamo wake, ambapo Halmashauri Kuu (NEC) ya CCM, iliyokutana juzi mjini Dodoma imetangaza msimamo wake ni kutetea hoja ya kuwa na Serikali mbili huku vyama vingine navyo kama Chadema na CUF vinataka Serikali tatu ilivyopendekezwa pia na Tume ya Mabadiliko ya Katiba.