APRM Yawataka Wajumbe Bunge la Katiba Kutanguliza Maslahi ya Taifa

Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano, wa APRM Hassan Abbas.

Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano, wa APRM Hassan Abbas.

MPANGO wa Afrika Kujitathmini Kiutawala Bora (APRM) tawi la Tanzania unatoa wito kwa wabunge wa Bunge Maalum la Katiba linaloanza Jumanne wiki hii mjini Dodoma kutanguliza maslahi bora ya Tanzania ya miaka mingi ijayo kuliko misimamo binafsi au matakwa ya taasisi wanazoziwakilisha.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa leo kwa vyombo vya habari na Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano, wa APRM Hassan Abbas, imewataka wajumbe kuvumiliana juu ya tofauti za kimtazamo, ambazo kwa hakika haziwezi kukosekana, hivyo ni vyema wabunge wakumbuke kanuni ya msingi katika ushawishi-nguvu ya hoja na si hoja ya nguvu.

“…Itakumbukwa kuwa APRM ni Mpango ulioasisiwa na viongozi wa Afrika kwa ajili ya kuhimiza utawala bora barani humu. Hivyo, mpango huu unapongeza hatua zilizofikiwa na Tanzania katika kuandika katiba mpya. Hatua hii ni ya kupigiwa mfano barani Afrika ambapo bara hili linasubiri kwa hamu kubwa hatma ya mchakato huu, alisema Abbas katika taarifa hiyo.

Alisema viongozi na wananchi wengi wa Afrika wanaichukulia Tanzania kuwa nchi ya mfano katika suala la amani, utulivu na utawala bora, na hali hii ilijidhihirisha pale Januari 2013 wakati Tanzania ilipowasilisha Ripoti yake ya APRM ambapo viongozi wengi wa Afrika waliipongeza Tanzania kwa kueleza kwa uwazi changamoto za ki-utawala zinazoikabili nchi na hatua zinazochukuliwa kukabiliana nazo.

“…Kwa kuwa tumefikia hatua nzuri katika uandaaji wa katiba yetu, na kwa kuwa madai ya kuwepo katiba mpya yamekuwepo kwa kipindi kirefu sasa, lengo likiwa ni kuboresha muundo wa utendaji, utawala bora na uwajibikaji; na kwa kuwa sasa kama Taifa tumeamua kuuhitimisha mchakato huu; APRM Tanzania inachukua fursa hii kutoa wito kwa wajumbe wa Bunge Maalum la Katiba kuweka alama yao muhimu katika mchakato huu wa kihistoria kwa kutimiza wajibu wao kizalendo na kwa kuzingatia matakwa ya wananchi kuliko hisia, mawazo au mitazamo binafsi ya kitaasisi katika kuijadili Katiba mpya,” alieleza katika taarifa hiyo.

Alisema APRM inaona umuhimu kwa wabunge wa Bunge la Katiba kukumbuka ukweli kwamba wananchi wengi walioshiriki kutoa maoni katika rasimu ya sasa ya Katiba walikuwa na mitazamo tofauti, hisia tofauti na hata imani tofauti, lakini wote walisimama kwa amani na imani moja kuu-kuijenga Tanzania bora zaidi ijayo.

“…Kwa sababu hizo basi sisi katika APRM tunatoa wito kwa wajumbe wote kutoka asasi na makundi mbalimbali waliopewa dhamana hii kuhakikisha kuwa wanajadili Katiba kwa minajili ya kuwapatia wananchi kile wanachokitarajia-Katiba itakayoboresha maisha yao.”

“APRM inatoa wito kuwa pale ambapo kutakuwa na tofauti za kimtazamo, ambazo kwa hakika haziwezi kukosekana, basi ni vyema wabunge wetu wakakumbuka kanuni ya msingi katika ushawishi-nguvu ya hoja na si hoja ya nguvu. Afrika inasubiri kujifunza kutoka kwetu, tuhakikishe kuwa faida hiyo inapatikana kwa kutumia vizuri fursa hii,” ilisema sehemu ya taarifa hiyo.