Na Mwandishi Maalumu
SHIRIKA la Maendeleo la Umoja wa Mataifa (UNDP) limeitaka Tanzania kuanzisha haraka awamu ya pili ya Operesheni Tokomeza yenye lengo la kukabiliana na kasi kubwa ya ujangili na mauaji ya wanyamapori katika Tanzania.
Aidha, Shirika hilo limesema kuwa linatambua na kupongeza juhudi zinazofanywa na Serikali ya Tanzania kupambana na ujangili, ikiwa ni pamoja na kuanzisha Operesheni Tokomeza kupambana na balaa la uwindaji haramu wa wanyamapori na biashara haramu ya meno ya tembo.
Shirika hilo pia limesema kuwa limekubali ombi la Tanzania la kuratibu jitihada za kimataifa za kuchangia fedha na raslimali nyingine za kuunga mkono juhudi za Tanzania kukabiliana na ujangili na kuiwezesha Tanzania kutelekeza malengo ya Mkakati wa Taifa wa kulinda maliasili na wanyapori.
Msimamo na pongezi hizo za UNDP zimetolewa asubuhi ya Februari 13, 2014, na Mkuu wa Shirika hilo la Umoja wa Mataifa, Hellen Clark wakati alipozungumza kwenye Mkutano wa Kimataifa wa Kupambana na Ujangili na Biashara Haramu ya Meno ya Tembo uliofanyika kwenye Jumba la Lancaster House mjini London, Uingereza.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Jakaya Mrisho Kikwete ameongoza ujumbe wa Tanzania ambako wakuu wa nchi na Serikali na wawakilishi wao kiasi cha 60 duniani wameshiriki.
Akizungumza kwenye Mkutano huo, Waziri Mkuu huyo wa zamani wa New Zealand amesema kuwa Serikali duniani zina wajibu wa kuongoza mapambano dhidi ya ujangili kupitia uratibu mkubwa zaidi wa taasisi mbali mbali za Serikali.
“Katika hili, UNDP inapenda kutambua hatua kubwa na kali ambazo zimeanzishwa na kuchukuliwa na Serikali ya Tanzania hasa kuanzisha Operesheni Tokomeza kukabiliana na ujangili na biashara haramu ya meno ya tembo,” amesema Mheshimiwa Clark na kuongeza:
“UNDP inapenda kuitaka Serikali ya Tanzania kuanzisha awamu ya pili ya Operesheni hiyo lakini kwa kuhakikisha kuwa awamu hiyo inatekelezwa kwa kutilia maanani kwa kiasi kikubwa viwango na taratibu za haki za binadamu.”
Bi. Clark ameongeza: “Isitoshe mafanikio katika kuzuia ujangili na biashara haramu ya meno ya tembo na hata faru yatapatikana tu iwapo Serikali na washirika wa kimataifa watakapotenga kiasi cha kutosha cha raslimali ili kuwezesha kupatikana kwa mabadiliko ya maana na ya haraka kutoka hali ya sasa.”
Ameongeza Bi. Clark: “ Baada ya kuwa tumechangia katika raslimali za kupata hesabu kamilifu ya tembo walio hai na kuunga mkono majadiliano ya karibuni kuhusu suala hili, UNDP inafurahi kutangaza kuwa imekubali ombi la Serikali ya Tanzania la kuratibu michango ya wabia wa maendeleo na kuunga mkono utekelezaji wa Mkakati wa Taifa wa kukabiliana na ujangili na kuhifadhi wanyamapori”.
Serikali iliendesha Operesheni Tokomeza Oktoba, mwaka jana, chini ya uongozi wa Jeshi la Wananchi wa Tanzania (TPDF) lakini Operesheni hiyo ilisimamishwa Novemba Mosi baada ya kutokea madai ya hitilafu za haki za binadamu katika uendeshaji wa Operesheni hiyo.
Wakati huo huo, Rais Jakaya Kikwete ameitaka Jumuia ya Kimataifa kusaidia kukomesha na kufunga masoko ya pembe za tembo na faru kama moja ya njia za kukomesha mauaji na biashara haramu ya wanyapori hawa.
Akizungumza Februari 13, 2014 kwenye Mkutano wa Kimataifa wa Kukabiliana na Ujangili na Biashara Haramu ya Pembe za Tembo kwenye Jumba la Lancaster mjini London, Rais Kikwete amesema kuwa bila kufunga masoko hayo kazi ya kudhibiti ujangili na mauaji ya wanyamapori hao itakuwa ngumu.
Rais Kikwete alikuwa mmoja wa viongozi wa Afrika ambao walizungumza kwenye ufunguzi wa Mkutano huo uliohudhuriwa na wakuu wa Serikali na nchi pamoja na wawakilishi wa nchi 60 duniani. Mkutano huo umeandaliwa na Serikali ya Uingereza kwa ombi la Mtoto wa Malkia wa Uingereza, Prince Charles.
Mbali na Rais Kikwete, viongozi wengine wa Afrika walioshiriki Mkutano huo na kuzungumza ni pamoja na Rais wa Botswana Jenerali Khama Iam Khama, Rais wa Gabon Ali Omar Bongo na Rais wa Chad Mheshimiwa Idrissa Deby. Ethiopia iliwakilishwa na Waziri.
Rais Kikwete amewaambia mamia ya wajumbe wa Mkutano huo: “Mwisho, nataka kuiomba Jumuia ya Kimataifa kuweka msimamo na kusaidia kukomesha biashara ya pembe za tembo na faru duniani. Kama hili litafanyika tembo na faru watakuwa salama.”
Ameongeza: “Wakati CITES ilipopiga marufuku biashara ya pembe za tembo mwaka 1989, hali hiyo ilisaidia kuongezeka kwa idadi ya tembo duniani. Naamini kuwa kama biashara hiyo itapigwa marufuku tena leo, matokeo yatakuwa yale yale. Maisha ya tembo na faru wengi yataokolewa na hatutakuwa na haja ya kuwa na wasiwasi.”
Rais pia ametoa mapendekezo mengine makuu manne kama njia ya kukabiliana na ujangili na biashara haramu ya pembe za ndovu ikiwa ni pamoja na ahadi kwamba Serikali itaendelea kuongeza nguvukazi ya maofisa na askari wanyamapori na kuhakikisha kuwa maofisa na askari hao wanapata mafunzo mwafaka ya kuifanya kazi hiyo.