Na Edson Kamukara
SIKU moja baada ya madiwa wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) jijini Arusha kugomea maamuzi ya Kamati Kuu (CC) ya chama hicho, yaliyowataka wajivue nyadhifa za Unaibu Meya na Uenyekiti wa Kamati mbili, Katibu Mkuu, Dk. Slaa ameibuka na kusema leo mchama hatma yao itajulikana.
Akizungumza na gazeti hili jana jijini Dar es Salaam, Dk. Slaa alisema kimsingi hakupaswa kusema lolote juu ya madai hayo ya madiwani wake hadi leo saa 7.02 mchana ambapo muda wa siku tatu walizopewa na CC kujivua nyadhifa hizo utakapokuwa umekoma.
Katika maagizo hayo ya CC, madiwani watatu wa CHADEMA Estomih Mallah (Naibu Meya), Rebeun Ngowi (Kamati ya kudumu ya Fedha na Utawala) na John Bayo (Kamati ya kudumu ya Elimu, Afya na Uchumi),waliagizwa kujivua nyadhifa hizo kutokana na chama Taifa kukataa kuafiki muafaka kwa madai haukuzingatia taratibu
Hatua hiyo, ilichukua sura mpya juzi baada ya madiwani wote 11 wa CHADEMA kutoa tamko kupitia kwa Mallah, wakidai hawaungi mkono maamuzi ya CC na hivyo wanaungana na wenzao watatu waendele na madaraka yao.
Katika tamko hilo, Mallah alisisitiza kuwa madiwani wa Arusha hawataki siasa za maji taka ambazo hazina manufaa na maslahi ya wananchi, huku akidai hakuna ushawishi wowote wa rushwa uliotumika ili kufikiwa kwa muafaka na wenzao wa CCM.
Walisema kuwa licha ya kupewa barua za kuwataka wajiuzulu, wanashangaa kuona chama hicho kimeshindwa hata kuwapa taarifa ya uchunguzi wa tume iliyoongozwa na Mabere Marando ili kufahamu kilichomo katika taarifa hiyo na waweze kujitetea mbele ya CC.
Kwamba iwapo tuhuma za rushwa dhidi yao zitashindikana kutolewa uthibitisho, watachukua hatua za kisheria kwa wale waliowatuhumu, akiwemo mbunge wa Jimbo la Arusha Mjini, Godbless Lema, wanayedai ndiye chanzo cha mgogoro.
Akifafanua madai hayo, Dk. Slaa alisema tamko la madiwani hao linapotosha jambo husika na badala yake wanachanganya mambo mawili yaani kosa la kukiuka maelekezo ya chama na mgogoro baina yao na mbunge wao Lema.
“Kimsingi, leo sikupaswa kusema chochote maana tuliwaandikia kuwaeleza kosa lao na kuwapa maagizo wajivue nyadhifa hizo ndani ya siku tatu, sisi hatufanyi kazi kupitia vyombo vya habari. Mwisho wa siku tatu walizopewa ni kesho (leo) saa 7.02, tusubiri kama watajibu kwa barua au la,” alisema Dk. Slaa.
Aliongeza kuwa kama hawatatimiza hilo basi hakutakuwa na msalie mtume isipokuwa taratibu na kanuni za chama zitafuatwa kulingana na katiba yao. Na kusisitiza kuwa CHADEMA haifanyi kazi kwa matakwa ya mtu.
Kuhusu madai ya tuhuma za rushwa na kunyimwa nafasi ya kujitetea katika CC, Dk. Slaa alisema hizo ni kauli za kutaka kupotosha suala husika kwani hata barua walizopewa hakuna mahali wanatuhumiwa kwa rushwa.
“Hili la rushwa, mimi kama Katibu Mkuu nililetewa malalamiko na hivyo ili kujiridhisha katika taarifa yangu kwa CC niliunda kamati ya kuchunguza tuhuma hizo kwa madiwani hao na ripoti iliyoletwa ni kwamba kamati ya Marando ilisema haikuweza kupata uwezekano wa kubaini kama kulikuwa na rushwa au la katika mchakato wa muafaka,” alisema Dk. Slaa.
Aliongeza kuwa, hata madai ya madiwani hao ya kunyimwa taarifa ya Marando si ya kweli kwani hawakuwahi kuomba, vile vile haikuwa na msingi sana kwani hiyo ilikuwa ni kamati ya kumshauri Katibu Mkuu wala haikuundwa na CC kama inavyoelezwa.
Dk. Slaa alisema kuwa alifanya juhudi binafsi za kuwaalika madiwani hao watatu wahudhurie kikao cha CC kilichopitisha maamuzi hayo, lakini licha ya kila mmoja kuthibitisha kuhudhuria, mwishowe hakuna aliyefika.
“Hata hivyo si kweli kama wanavyodai kuwa CC ni chombo cha mwisho, hivyo hawana mahala pa kukata rufaa. Bado kuna chombo kingine cha Baraza kuu, ambaye anahisi hakutendewa haki, anaweza kukata rufaa,” alisema na kuongeza kuwa;
Baadhi ya madiwani hao wanachanganya migogoro kwa kulinganisha mambo mawili. Kwamba wana mgogoro na Lema halafu wanadhani CC inawataka wajiuzulu kwa vile wanatofautia na mbunge.
Dk. Slaa alibainisha kuwa mgogoro huo wa Lema na baadhi ya madiwani umemfikia na tayari amemwandikia mbunge huyo barua ajieleze. Hivyo akawataka madiwani hao kutochanganya mgogoro huo na sakata la kufikia muafaka kinyume na maagizo.
Alisema CHADEMA inaukataa muafaka wa Arushwa kwa vile ulikiuka taratibu za vyama vyote viwili, na kufanya hivyo ni kuhalalisha kuwa chama hicho kilikuwa kinapigania nafasi hzio za unaibu meya na kamati.