Watuhumiwa 70 Wahusishwa na Ugaidi Nchini Kenya

Rais wa Kenya, Uhuru Kenyatta

Rais wa Kenya, Uhuru Kenyatta

RAIA 70 waliokamatwa hivi karibuni Jijini Mombasa Kenya, katika fujo zilizotokea kwenye Msikiti wa Musa wameshitakiwa katika mahakama ya Mombasa na kukutwa na kesi ya kujibu dhidi ya tuhuma zinazowakabili. Raia hao wanakabiliwa na mashitaka saba yanayohusiana na ugaidi yakijumuishwa kuwa wanachama wa kundi la kigaidi la Al Shabaab na wamewekwa rumande hadi Februari 26 ambapo mahakama itatoa uamuzi kuhusu ombi la wakili wao kutaka waachiwe kwa dhamana au la.

Baada ya kuzuiliwa na polisi kwa takriban siku kumi, washukiwa hao walipelekwa katika mahakama ya Mombasa lakini walikana mashtaka yao saba yanayowakabili mbele ya Hakimu, Richard Odenyo. Mbali na ugaidi washtakiwa hao wanakabiliwa na makosa mengine ya kumiliki silaha kinyume cha sheria, wizi wa kutumia mabavu na uchochezi. Washtakiwa hao ni miongoni mwa raia 104 waliokuwa wamezuiliwa awali kabla ya 33 kuachiwa jana baada ya serikali kuwaondolea mashtaka ya ugaidi na wizi wa kutumia nguvu kwa kukosekana ushahidi.

Mawakili wa washtakiwa hao Mohammed Balala na Mureithi Mbugua waliwasilisha ombi mahakamani kutaka waachiliwe kwa dhamana lakini upande wa mashtaka ukapinga ukisema kuwa walikuwa hatari kwa usalama wa taifa. Hii ni moja ya kesi ambayo inamvuto zaidi kwa misingi kuwa Serikali ya Kenya imehusisha Msikiti Musa kwa kutoa mafunzo ya misimamo mikali miongoni mwa vijana wakiambiwa kuwa ni Jihad ama vita vitakatifu.

Inadaiwa kuwa vijana wanaoshiriki sala katika msikiti huo wamekuwa wakisajiliwa na kuelelekea Somalia kujiunga na kundi la ugaidi la Al Shabab. Kutokana na kukamatwa kwa washukiwa hao msikitini viongozi wa dini ya kiislamu walishutumu maafisa wa polisi kuingia msikitini na viatu . Watu wawili waliuawa katika makabiliano hayo

Serikali ya Rais Uhuru Kenyatta imeahidi kupambana vilivyo dhidi ya makundi ya vijana wapiganaji wanaosema wanafanya hivyo kwa lengo la kidini. Kundi la wanamgambo la Al Shabaab lilikiri kufanya mashambulizi ya kigaidi dhidi ya jengo la kifahari la maduka la Westgate na kuwaua wakenya 67 mjini Nairobi mwezi Septemba mwaka jana. Serikali imesema kuwa haitakubali maeneo ya maombi kutumiwa kama vituo vya kuhubiri itikadi kali za kidini.

-DW