Wanaharakati Walalamikia Uteuzi Wajumbe Bunge la Katiba

Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa TGNP, Lilian Liundi akizungumza.

Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa TGNP, Lilian Liundi akizungumza.


Na Mwandishi Wetu

WANAHARAKATI wa masuala ya kijinsia, haki za binadamu, demokrasia na utawala bora wameulalamikia uteuzi wa wajumbe maalumu wa bunge la katiba uliofanywa hivi karibuni kwa madai idadi kubwa ya wajumbe katika bunge hilo wamejazwa wanasiasa na hivyo kukosa uwakilishi wa kutosha wa makundi yote.

Hivi karibuni Rais Jakaya Kikwete alitangaza majina ya wajumbe 201 wa Bunge la Katiba, watakaoshirikiana na wajumbe wengine  ambao ni wabunge wote wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania wapatao 357, wajumbe wa Baraza la wawakilishi Zanzibar wapatao 81 na kufanya jumla kuu ya wajumbe kuwa 639 watakao shiriki bunge maalum la katiba.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na wanaharakati hao na kusainiwa na Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa TGNP Mtandao, Lilian Liundi; licha ya wao kupendekeza  majina ya wataalamu wa masuala ya kijinsia na haki za binadamu ambao wangeshiriki kutetea baadhi ya vifungu vya rasimu ambavyo vinabeba sauti za wananchi kwa mustakabali wa taifa mapendekezo yao hayakuzingatiwa.

Taarifa hiyo imebainisha kuwa mchakato huo wa uteuzi umekuwa na mapungufu na sura tofauti kama ilivyokuwa katika kipindi cha kujadili Muswada wa Sheria ya Marekebisho ya Sheria ya Mabadiliko ya Katiba 2013.

Imefafanua kuwa miongoni mwa dosari za uteuzi ni kukosekana kwa ushiriki mpana wa uwakilishi wa makundi halisi yaliyoko pembezoni na kuchomeka majina ya watu wasiostahili kwenye nafasi za makundi mengine kutasababisha mapungufu makubwa ya uwakilishi katika mchakato huu.

“…Tumesikitishwa na kuingizwa kwa majina ya wanasiasa kwenye  kundi la NGO na kuwaacha wawakilishi wa asasi za kiraia wakati wanasiasa walikuwa na uwakilishi mkubwa kwenye kundi lao la watu 40. Aidha kundi la watu wenye mlengo unaofanana nalo hatukupewea tafsiri  halisi kuwa ni watu kuitoka kundi gani au ni kina nani badala yake wameingia wanasiasa na kulifanya Bunge hili la katiba kuwa na wanasiasa wengi  zaidi ya makundi mengine,” ilisema taarifa hiyo.

Aidha taarifa imehoji ni kwanini wanasiasa hawakuteuliwa tu kupitia kundi lao la wajumbe 40 na badala yake wao kuingizwa kupitia kundi la watu wenye malengo yanayofanana hivyo kuchukua nafasi za walengwa wengine.

“…Tunajiuliza kwa hali hii ya kujaza wanasiasa kwenye haya makundi ya wananchi tutapata katiba mpya tunayostahili kuwa nayo? Tunadai uwakilishi zaidi wa makundi mengine kwenye hili Bunge kwa sababu:- Wabunge wa sasa hawakuchaguliwa kwa kuzingatia uwiano wa kijinsia na makundi yaliyoko pembezoni,  Wabunge wa sasa wamechaguliwa kwa kuzingatia mfumo na ushawishi na itikadi za vyama vyao vya siasa; na sifa  zilizopelekea kuchaguliwa kwao na hadidu zao za rejea zimejikita katika kusimamia na kutetea katiba iliyopo na siyo kitunga Katiba.”

“…Tunaendelea kudai usawa wa Kijinsia katika mchakato huu kwani msingi wa kijinsia haujazingatiwa kama vile Itifaki ya Maputo, AU Constituent Act, AU Shared Values na CEDAW na Mkataba wa Watoto (CRC) zinavyotamka. Pia tunataka masuala muhimu ya wanawake ambayo yameonekana kwenye rasimu ya pili ya Katiba yaheshimiwe na wajumbe wa Bunge hili na yasitolewe bali yaboreshwe ili kutoa nafasi ya ushiriki kamili wa wanawake na wanaume  katika mgawanyo wa rasilimali za Taifa na kwenye fursa za uongozi,” ilisema taarifa hiyo ya wanaharakati anuai.