Tahadhari Kutoka Hali ya Hewa: Mvua Kubwa, Upepo Mkali na Mawimbi Makubwa Pwani

Ukanda wa pwani

Ukanda wa pwani


TAHADHARI imetolewa na Mamlaka ya Hali ya Hewa nchini (TMA) ya kuwepo kwa Vipindi vya Mvua kubwa, Upepo Mkali na Mawimbi Makubwa yatakayojitokeza ukanda wa mikoa ya Pwani yaani, Tanga, Dar es Salaam, Pwani, Lindi, Mtwara pamoja na visiwa vya Unguja na Pemba.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na TMA leo jijini Dar es Salaam maeneo mengine yatakayo athiriwa na hali hiyo ni pamoja na mikoa ya Mbeya, Njombe, Ruvuma pamoja na kusini mwa mkoa wa Morogoro.

Ikifafanua zaidi taarifa hiyo ilibainisha kuwa vipindi vya mvua kubwa zenye ujazo wa zaidi ya mm 50 ndani ya saa 24 zitanyesha huku zikiambatana na hali ya Upepo mkali unaozidi kilomita 40 kwa saa pamoja na mawimbi makubwa zaidi ya mita 2.0.

“…Maeneo yanayotarajiwa kuathirika na mvua kubwa ni Ukanda wa Pwani mikoa ya Tanga, Dar es Salaam, Pwani, Lindi, Mtwara pamoja na visiwa vya Unguja na Pemba. Upepo Mkali na Mawimbi Makubwa yatavuma Pwani ya mikoa ya Tanga, Dar es Salaam, Pwani, Lindi, Mtwara pamoja na visiwa vya Unguja na Pemba,” ilisema taarifa hiyo ya TMA.

“Hali hii inatokana na kuwepo kwa kimbunga “FOBANE” kusini magharibi mwa Bahari ya Hindi. Mfumo huu unatarajiwa kuvuta upepo kutoka Pwani ya Somalia na misitu ya Congo kuelekea maeneo ya nchi yetu,” ilisema taarifa hiyo.

Hata hivyo angalizo limetolewa kwa watumiaji wa bahari na wakazi wa maeneo hatarishi, hivyo wanashauriwa kuchukua tahadhari. Imebainisha kuwa Mamlaka ya Hali ya Hewa inaendelea kufuatilia hali hii na itatoa mrejeo pale itakapobidi.