Serikali Rombo Kuwaadhibu Watendaji Wanaohujumu Mazingira

Picha inayoonesha eneo la Rongai, Rombo

Picha inayoonesha eneo la Rongai, Rombo

Na Yohane Gervas, Rombo

MKUU wa Wilaya ya Rombo, Elinas Palengyo amesema Serikali haitasita kuwachukulia hatua kali watendaji wote wa kijiji watakao thibitika kuwa wanakwamisha juhudi za Serikali za utunzaji wa mazingira kwa kupokea rushwa na kutoa vibali vya kukata miti katika maeneo yao.

Mkuu wa wilaya ametoa kauli hiyo jana wakati alipokuwa akizungumza na dev.kisakuzi.com ofisini kwake, ambapo alisisitiza agizo lililotolewa na hivi karibunu na Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, Leonidas Gama la kuzuia vibali vya kukata miti litafanikiwa iwapo watendaji hao watafanya kazi kwa uadilifu na kuzingatia sheria.

Alisema kuwa hadi sasa wanawashikilia wenyeviti wawili wa vijiji, waliokuwa wakidaiwa kuharibu mazingira na kutoa vibali vya kukata miti kinyume na agizo la Serikali.

Aidha Pallengyo amesema kuwa wanaendelea kuwahamasisha wananchi kutumia nishati mbadala ikiwemo Gesi na bayogesi ili kulinda mazingira. Pia ametoa wito kwa wakazi wa Wilaya ya Rombo kutoa taarifa pale wanapoona viongozi au wananchi wanaoharibu mazingira ili wachukuliwe hatua za kisheria.

Aidha alisema juhudi hizo za kuhamasisha wanachi utunzaji wa mazingira na hasa kutokata miti ni changamoto lakini akasema kuwa wananchi wanapaswa kuelewa kuwa serikali ilifanya hivyo ikiwa na malengo mazuri.