Na Ronald Ndungi, EANA- Arusha
TAASISI ya Kimataifa ya Fedha (IFC) imetiliana saini makubaliano ya dola za Kimarekani milioni 3.9 sawa na Sh. bilioni 6.2 za Tanzania zitakazotumika kutoa bima kwa wakulima wapatao milioni moja katika nchi wananchama wa Jumuiya ya Afrika mashariki (EAC) kwa kipindi cha miaka miwili.
Kiongozi wa Kanda wa IFC, David Crush aliwaambia waandishi wa habari mjini Nairobi, Kenya kwamba mfuko huo utaanzisha bima ya mazao na mifugo utakaowezesha wakulima kukabiliana na athari za mabadiliko ya hali ya hewa.
“Mwaka huu wa 2014 tutatoa bima kwa wakulima wadogo angalau 500,000 katika nchi za Kenya, Rwanda na Tanzania,” Crush alisema wakati wa hafla ya utiaji saini Jumatano.
Fedha hizo zitatolewa na kampuni ya Global Index Insurance Facility, mfuko wa ambao unafadhiliwa na Umoja wa Ulaya (EU), Japani na Netherlands na kutekelezwa na IFC na Benki ya Dunia (WB). Mwaka jana wakulima wadogo 189,000 walipatiwa bima hiyo kupitia mradi huo.
Alifafanua kwamba Tanzania itajiunga na mpango huu mwaka huu.
“Tumemaliza hivi karibuni upembuzi yakinifu nchini Tanzania kuhusu bima ya mazao ambao ulichambua taarifa za historia ya hali ya hewa,” alisema.
Crush alisema kwamba wataanza pia upembuzi yakinifu juu uwezekano wa kuazisha pia mradi kama huo nchini Uganda katika kipindi cha miezi michache ijayo.
Alisema kwamba bima itolewayo inayolenga mabadiliko ya hali ya hewa inaweza kumlinda mkulima dhidi ya athari za hali mbaya ya mabadiliko ya hali ya hewa na pia kuimarisha usalama wa chakula kwa jamii za vijijini.
“Huu ni uboreshaji wa bima ya kilimo cha jadi kinachotegemea usimamizi wa hasara inayotokana na kilimo ambayo kiwango chake hupatikana kutokana ukaguzi wa mashamba,” Kiongozi huyo wa Kanda alisema.