Dk Gharib Bilal Ampokea Balozi Mpya wa Oman Tanzania

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. Mohammed Gharib Bilal, akiagana na Balozi mpya wa Oman nchini Tanzania, Soud Ali Mohamed Al Ruqaishi, baada ya mazungumzo yao yaliyofanyika ofisini kwa Makamu Ikulu jijini Dar es Salaam, leo Feb 7. Picha na OMR

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. Mohammed Gharib Bilal, akiagana na Balozi mpya wa Oman nchini Tanzania, Soud Ali Mohamed Al Ruqaishi, baada ya mazungumzo yao yaliyofanyika ofisini kwa Makamu Ikulu jijini Dar es Salaam, leo Feb 7. Picha na OMR

MAKAMU wa Rais Dk. Mohammed Gharib Bilal amempokea Balozi mpya wa Oman nchini Tanzania Balozi Soud Ali Mohamed Al Ruqaishi ofisini kwake Ikulu Jijini Dar es Salaam na kisha kufanya naye mazungumzo. Katika mazungumzo hayo, Makamu wa Rais amemhakikishia Balozi Ruqaishi kuwa Tanzania na Oman zina uhusiano wa kindugu wa siku nyingi na kwamba uhusiano huo umekuwa ukinufaisha nchi hizi kwa miaka kadhaa. 

Makamu wa Rais aliendelea kufafanua kuwa, Tanzania kwa sasa inashirikiana na Oman kiuchumi na kwamba kuna wawekezaji wengi kutoka Oman ambao wako nchini, sambamba na wengine wanaoonesha nia ya kuwekeza katika sekta mbalimbali hapa Tanzania.

Kwa upande wake Balozi Ruqaishi alimueleza Makamu wa Rais kuwa, Oman inafurahia uhusiano wake na Tanzania na kwamba jukumu lake la kwanza ni kuhakikisha kuwa uhusiano huo unadumu na kunufaisha nchi hizi mbili. Pili alifafanua kuwa, atahakikisha katika kipindi chake cha Ubalozi hapa Tanzania anasaidia kutanua fursa za uwekezaji kwa wawekezaji kutoka Oman sambamba na kuwafungulia fursa kama hizo wawekezaji walio na nia ya kuwekeza nchini Tanzania. 

Oman licha ya kuwa na uhusiano wa karibu na Tanzania na hasa Visiwani Zanzibar, inabakia kuwa ndiyo nchi pekee duniani nje ya Afrika iliyo na wazungumzaji wengi wa lugha ya Kiswahili. Katika siku za hivi karibuni, wawekezaji kutoka Oman wameonesha nia ya kuwekeza katika sekta ya Mafuta na Gesi sambamba na kuliimarisha shirika la Ndege Tanzania ili limudu ushindani na kuongeza ufanisi wa shughuli zake katika biashara ya safari za anga.
Imetolewa na: Ofisi ya Makamu wa Rais Dar es Salaam, Februari 07, 2014.