Rais Kikwete Afungua Mkutano wa Baraza la Vyama vya Siasa

Rais Jakaya Mrisho Kikwete akiwa na Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Maalim Seif Shariff Hamad, Msajili wa vyama vya siasa Jaji Francis Mutungi na viongozi wa vyama mbalimbali vya siasa na maafisa wa serikali wakitoka kupata chakula cha mchana baada ya kufungua mkutano wa Baraza la Vyama vya Siasa Februari 6, 2014 katika Ukumbi wa Mikutano wa Mwalimu Nyerere jijini Dar es salaam

Rais Jakaya Mrisho Kikwete akiwa na Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Maalim Seif Shariff Hamad, Msajili wa vyama vya siasa Jaji Francis Mutungi na viongozi wa vyama mbalimbali vya siasa na maafisa wa serikali wakitoka kupata chakula cha mchana baada ya kufungua mkutano wa Baraza la Vyama vya Siasa Februari 6, 2014 katika Ukumbi wa Mikutano wa Mwalimu Nyerere jijini Dar es salaam

Rais Kikwete Afungua Mkutano wa Baraza la Vyama vya Siasa

Sehemu ya viongozi wa vyama mbalimbali vya siasa katika mkutano wa Baraza la Vyama vya Siasa Februari 6, 2014 katika Ukumbi wa Mikutano wa Mwalimu Nyerere jijini Dar es salaam.

Sehemu ya viongozi wa vyama mbalimbali vya siasa katika mkutano wa Baraza la Vyama vya Siasa Februari 6, 2014 katika Ukumbi wa Mikutano wa Mwalimu Nyerere jijini Dar es salaam.

Sehemu ya viongozi wa vyama mbalimbali vya siasa wakiomba dua kabla ya kuanza kwa mkutano wa Baraza la Vyama vya Siasa Februari 6, 2014 katika Ukumbi wa Mikutano wa Mwalimu Nyerere Rais Kikwete Afungua Mkutano wa Baraza la Vyama vya Siasajijini Dar es salaam.

Sehemu ya viongozi wa vyama mbalimbali vya siasa wakiomba dua kabla ya kuanza kwa mkutano wa Baraza la Vyama vya Siasa Februari 6, 2014 katika Ukumbi wa Mikutano wa Mwalimu Nyerere Rais Kikwete Afungua Mkutano wa Baraza la Vyama vya Siasajijini Dar es salaam.

Rais Jakaya Mrisho Kikwete akiwa na Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Maalim Seif Shariff Hamad, Msajili wa vyama vya siasa Jaji Francis Mutungi na viongozi wa vyama mbalimbali vya siasa na maafisa wa serikali wakitoka kupata chakula cha mchana baada ya kufungua mkutano wa Baraza la Vyama vya Siasa Februari 6, 2014 katika Ukumbi wa Mikutano wa Mwalimu Nyerere jijini Dar es salaam

Rais Jakaya Mrisho Kikwete akiwa na Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Maalim Seif Shariff Hamad, Msajili wa vyama vya siasa Jaji Francis Mutungi na viongozi wa vyama mbalimbali vya siasa na maafisa wa serikali wakitoka kupata chakula cha mchana baada ya kufungua mkutano wa Baraza la Vyama vya Siasa Februari 6, 2014 katika Ukumbi wa Mikutano wa Mwalimu Nyerere jijini Dar es salaam

cc6-

HOTUBA YA MHESHIMIWA JAKAYA MRISHO KIKWETE, RAIS WA JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA KWENYE KIKAO CHA BARAZA LA VYAMA VYA SIASA, UKUMBI WA MIKUTANO WA KIMATAIFA WA MWALIMU NYERERE, TAREHE 6 FEBRUARI, 2014 DAR ES SALAAM

Ndugu Peter Mziray, Mwenyekiti wa Baraza la Vyama vya Siasa;
Ndugu Vuai Ali Vuai, Makamu Mwenyekiti wa Baraza la Vyama vya Siasa;
Mheshimiwa Jaji Francis Mutungi, Msajili wa Vyama vya Siasa;
Ndugu Wenyeviti wa Vyama vya Siasa;
Ndugu Wajumbe wa Baraza la Vyama Siasa;
Wageni Waalikwa;
Mabibi na Mabwana;
Utangulizi
Nakushukuru ndugu Peter Mziray, Mwenyekiti wa Baraza la Vyama vya Siasa na viongozi wenzako kwa kunishirikisha kwenye kikao hiki maalum cha Baraza na kwa maelezo mazuri ya utangulizi. Tutayatafakari ya kufanyika yafanyike. Nawapongeza kwa uamuzi wenu wa busara wa kuzungumzia nafasi ya vyama vya siasa katika Bunge Maalum la kutunga Katiba. Jambo hili ni muhimu kwa uhai, maendeleo na ustawi wa nchi yetu na watu wake. Mmeonesha moyo wa uzalendo na ukomavu wa kisiasa wa hali ya juu
Tangu Baraza hili la vyama vya siasa lizinduliwe mwezi Mei, 2010, nimekuwa nikifuatilia kwa karibu shughuli zake na jinsi linavyofanya kazi. Kwa kweli nimeridhishwa na hatua mliyopiga. Ndiyo maana mliponiita sikusita kuja. Nawaahidi kuwa nitaendelea kufanya hivyo katika siku zijazo ili mradi tu nafasi iwepo.
Serikali Kuimarisha Uwanja wa Siasa
Ndugu Wajumbe;
Mtakubaliana nami kuwa Tanzania imepiga hatua kubwa katika kujenga na kuendeleza demokrasia ya vyama vingi na ushindani wa kisiasa. Kuwepo kwa vyama 21 vyenye usajili wa kudumu vilivyo huru kuendesha shughuli zao na Baraza la Vyama vya Siasa ni kielelezo tosha cha ukweli huu. Wazo la kuwa na Baraza hili liliibuka wakati wa mchakato wa kutatua mgogoro wa kisiasa wa Zanzibar uliozuka baada ya Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2000. Kamati ya Pamoja ya Mwafaka iliyokuwa na wajumbe kutoka CCM na CUF iliundwa ili kutafuta suluhu ya mgogoro ule. Mojawapo ya mambo ambayo Kamati hiyo ilipendekeza ni kuundwa kwa chombo kitachowezesha viongozi wa vyama vya siasa kukutana mara kwa mara kujadili masuala ya kisiasa ili kuepusha migogoro ya kisiasa.
Baada ya Baraza kuundwa, mwaka 2009, Serikali ikaona haja ya kupanua wigo wa ushiriki na kukifanya chombo hiki kuendesha kazi zake kwa mujibu wa Sheria. Matokeo yake Wenyeviti wa vyama vyote vya siasa wakajumuishwa kufuatia marekebisho ya Sheria ya Vyama vya Siasa yaliyofanyika mwaka 2009. Baraza la Vyama vya Siasa likatambulika kisheria na majukumu yake kuorodheshwa katika Sheria husika. Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa ikapewa jukumu la kuratibu na kugharimia shughuli za Baraza la Vyama vya Siasa.
Mabibi na Mabwana;
Nimeamua kueleza chimbuko la Baraza la Vyama vya Siasa, ili Wajumbe wa Baraza na watu wote wanaonisikiliza wajue kwamba Baraza hili limetokeaje kuwepo na lina nafasi gani katika jamii na siasa za Tanzania. Ni chombo kilichotokana na mafunzo tuliyopata katika migogoro ya kisiasa huko nyuma. Baraza hili ndicho chombo ambacho kikitumiwa vizuri na vyama vya siasa matatizo na malalamiko yao na masuala mengine ya kisiasa yana mahali pa kujadiliwa na kupatiwa ufumbuzi. Aidha, ni jukwaa linalotoa fursa kwa vyama vya siasa kuzungumzia masuala mbalimbali yenye maslahi kwa taifa na kukubaliana kuhusu nini vyama vyenyewe vifanye au vishauri yafanyike na mamlaka husika. Ushauri unaotolewa unawasilishwa Serikalini kupitia Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa ambayo ndio Sekretarieti ya Baraza hili.
Hakuna chombo kingine zaidi ya Baraza hili kinachowakutanisha viongozi wote wa kitaifa wa vyama vya siasa kujadili masuala ya kisiasa yenye maslahi ya kitaifa. Kwa kuzingatia nafasi yake na majukumu ya Baraza hili, nawasihi viongozi wenzangu hususan Wenyeviti wa vyama vya siasa tulipe uzito na tulitumie ipasavyo. Nawaomba tuwe tunashiriki kwa ukamilifu katika vikao na shughuli za Baraza. Natambua kwamba kwa vile Baraza linajumuisha vyama vyote hata Mwenyekiti wa Chama kidogo anaweza kuongoza Baraza inaweza kutokupendeza kwa vyama vikubwa. Si jambo la ajabu wala si jambo baya ndiyo maana na faida ya demokrasia. Wale wanaotoka vyama vikubwa wasichukie, wakifanya hivyo wanakiuka kanuni moja ya msingi ya uongozi nayo ni “kiongozi mzuri pia huwa ni mfuasi mzuri”. Hata mdogo analo la maana la kuwanufaisha wote wadogo na wakubwa. Naamini Baraza likitumika vizuri litatunufaisha wote: vyama vyote, nchi yetu na wananchi wote.
Mimi na Mheshimiwa Ali Mohamed Shein, Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi kwa nafasi zetu hatushiriki moja kwa moja katika mikutano ya Baraza hili. Pamoja na hilo bado tunalitambua, tunalithamini na tunayachukulia maamuzi ya Baraza hili kwa uzito unaostahili. Ndiyo maana Chama changu kimemteua kiongozi mzito anayenifuata kwa madaraka yaani Makamu Mwenyekiti, ndugu Philip Mangula kuwa Mjumbe wa Baraza. Kutoka Zanzibar tumemteua Naibu Katibu Mkuu wa CCM, Ndugu Vuai Ali Vuai.
Kwa kweli ingependeza sana kama viongozi wa vyama vingine nao wangetoa uzito unaostahili kwa Baraza hili. Natoa rai kwa viongozi wakuu wa vyama vya siasa, hususan wenyeviti kwa wao wenyewe kuwa Wajumbe wa Baraza hili adhimu ili kulipa uzito na hadhi stahiki. Baraza hili lilianzishwa kwa ajili yetu, kujadili masuala ya kuimarisha na kuboresha uwanja wa siasa nchini na kuweka mazingira na uwanja ulio huru na sawa. Kusudi la kutaka wenyeviti wote wa kitaifa wa vyama vya siasa wawe wajumbe wa Baraza ni kuhakikisha kuwa Baraza linakuwa na uwakilishi wa watu wenye mamlaka kamili kufanya maamuzi kwa niaba ya vyama vyao. Ni muhimu sote tuone hoja hiyo na kuitumia fursa inayotolewa na Baraza. Napenda kuwahakikishia ndugu wajumbe kuwa Serikali itaendelea kusikiliza na kuheshimu ushauri wa Baraza hili kwani ni chombo muhimu sana kwa mustakabali wa ustawi wa siasa na maendeleo ya nchi yetu.
Ndugu Wajumbe wa Baraza la Vyama vya Siasa;
Jambo lingine muhimu tunaloendelea kufanya ni kuimarisha Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa ili iweze kumudu vyema majukumu yake. Mwaka jana (2013) niliidhinisha muundo mpya wa Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa wenye vitengo vingi kuliko ilivyokuwa kabla ya hapo. Muundo mpya unaoongozwa na watumishi wenye taaluma nyingine mbalimbali badala ya kutegemea wanasheria peke yake. Changamoto zinaongezeka na mazingira ya kufanya kazi yanabadilika, hivyo Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa itafaidika na kuwa na watumishi wa kada nyingine kama vile wa sosholojia, sayansi ya siasa na kadhalika.
Ili kuhakikisha ufanisi zaidi, Serikali imedhamiria kuongeza bajeti ya ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa katika mwaka ujao wa fedha. Bila ya kufanya hivyo tutakuwa hatukufanya kitu cha maana. Ofisi haitaweza kutimiza wajibu wake. Kwa kweli itakuwa ni kuwaonea kuwadai wafanye zaidi.
Ndugu Mwenyekiti na Wajumbe wa Baraza la Vyama vya Siasa;
Nimeelezwa na Msajili wa Vyama vya Siasa kuwa, jambo moja linaloikwaza ofisi yake ili waweze kutimiza ipasavyo jukumu lao la kuwa mlezi wa vyama vya siasa nchini ni mfumo wa Sheria ya Vyama vya Siasa. Nimeelezwa kuwa Sheria hii imeweka adhabu moja tu ambayo ni kukifuta Chama kinachofanya makosa yaliyoainishwa katika Sheria badala ya kutafuta taratibu za kurekebisha. Kwa maoni yake Sheria haitoi nafasi ya kutosha ya kuvilea vyama vikue, vikomae na vijiepushe na migogoro ya kisiasa ndani ya vyama na ndani ya jamii. Kwa sababu hiyo, inamfanya Msajili aonekane kuwa ni mtu wa kutoa vitisho vya kufungia vyama. Kwa maoni yake hatuna budi kuangalia sheria hiyo upya ili iweze kushughulikia changamoto hizo.
Naiona hoja ya Msajili na nampongeza sana kwa kuliona jambo hilo. Leteni mapendekezo yenu tuyatazame ili hatua zipasazo zichukuliwe. Pamoja na hayo usisubiri sheria. Mlezi hutoa ushauri na kusaidia kupata ufumbuzi wa mambo mbalimbali yanayowatatiza viongozi na wanachama wa vyama vya siasa. Usisite kututembelea mara kwa mara kuzungumza nasi na kutushauri unavyoona inafaa. Itasaidia sana wakati tunasubiri Sheria kufanyiwa marekebisho. Nafurahi kwamba kazi hiyo unaifanya. Tafadhali endelea. Pia usisite kutuita wote au mmoja mmoja unapoona inafaa kufanya hivyo.
Nimeambiwa mchakato wa kupitia upya Sheria hiyo na ile ya Gharama za Uchaguzi umeanzishwa na Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa. Bila ya shaka marekebisho ya Sheria ya Vyama yatasaidia kuboresha uratibu wa shughuli za kisiasa hapa nchini bila kuingilia uhuru wa vyama vya siasa. Vilevile marekebisho ya Sheria ya Gharama za Uchaguzi yatasaidia kuhakikisha wananchi wetu wanachagua viongozi kwa kuzingatia uwezo wao, mwenendo na ubora wa sera za vyama vyao na si uwezo wao wa kifedha. Nimefurahi na nimefarijika sana na hatua hiyo. Ongezeni kasi ya kukamilisha zoezi hilo.
Ndugu Washiriki;
Naomba kurudia tena kusema kuwa tunafanya hayo yote ili kuimarisha demokrasia ya vyama vingi na ushindani wa kisiasa nchini. Kwetu sisi Serikalini, vyama vya siasa ni wadau muhimu wa maendeleo ya nchi yetu na watu wake. Kwa maana hiyo tunapenda vyama viwe na uwezo wa kutekeleza wajibu huo. Kinyume chake, yaani vyama vinaweza kugeuka na kuwa wakala wa kurudisha nyuma maendeleo. Hii haikubaliki, itashangaza na kusikitisha.

Mada ya Kikao
Ndugu Mwenyekiti;
Kama wote mnavyofahamu, nchi yetu ipo katika mchakato wa kuandika Katiba Mpya. Hatua inayofuatia sasa ni Bunge Maalum la Katiba kukutana na kujadili Rasimu ya Pili na kuamua ipasavyo. Kazi ya uteuzi wa Wajumbe 201 wa kuungana na Wabunge na Wawakilishi katika Bunge hilo imekamilika na kesho watatangazwa. Ilikuwa kazi ngumu sana. Watu wengi wazuri walipendekezwa hivyo hujui umchague nani na umuache nani. Kwa vile hatuwezi kuwapeleka wote basi tumewateua hao 201 na kuwaacha maelfu ya watu wazuri. Kama wote wanaofaa wangechukuliwa nchi ingenufaika sana. Lakini hatuwezi kuwa na Bunge la watu 5,000 hata China haifanyi hivyo. Ilikuwa hapana budi kuchagua baadhi yao tu. Kwa ajili hiyo nawasihi wale wote wasioteuliwa wasisononeke. Hawajapungukiwa sifa ila nafasi hazitoshi.
Ndugu Wajumbe;
Wiki iliyopita nilitembelea ukumbi wa Bunge Dodoma na kujionea mwenyewe maandalizi ya Ukumbi na vifaa unavyoendelea. Mambo yanakwenda vizuri. Nimeelezwa kuwa ifikapo tarehe 10 Februari, 2014 kila kitu kitakuwa tayari na majaribio kufanywa ya vifaa vilivyofungwa. Nimeona tujipe wiki moja baada ya hapo ili tuweze kurekebisha panapostahili. Kwa ajili hiyo nimekubaliana na Rais wa Zanzibar niangalie uwezekano wa kuliitisha Bunge Maalum tarehe 18 Februari, 2014. Tutaitangaza rasmi siku hiyo kupitia gazeti la Serikali.
Bunge la Katiba ndilo lenye mamlaka ya kutunga Katiba mpya ya nchi yetu. Hatua zote zilizopita ni za kutoa mapendekezo jukumu ambalo Tume ya Mabadiliko ya Katiba imelikamilisha vyema. Ipo Rasimu ya Katiba itakayofikishwa kwenye Bunge Maalum kujadiliwa na kufanyiwa uamuzi. Ingekuwa Bunge la kawaida au Baraza la Wawakilishi, Rasimu ya Katiba ndiyo Muswada wa Sheria utakaofikishwa Bungeni na kwenye Baraza.
Wajumbe wa Bunge hilo watambue kuwa wana dhamana isiyokuwa na mfano wake kwa nchi yetu na Watanzania wenzao kwa jumla. Wanalo jukumu la kuwapatia Katiba nzuri itakayodumu kwa zaidi ya miaka 50 ijayo. Katiba itakayoimarisha Muungano badala ya kuudhoofisha. Katiba itakayodumisha umoja, amani na utulivu nchini badala ya kuvuruga. Vilevile Katiba itakayoweka mazingira mazuri ya kisiasa, kijamii na kiuchumi na kuongeza kasi ya maendeleo ya nchi yetu na ustawi wa watu wake kwa miaka mingi ijayo. Ili haya yafanyike ni vyema Wajumbe wajue vyema kinachopendekezwa, wapambanue kinachofaa na kisichofaa, na kubwa zaidi, watangulize maslahi ya taifa mbele kuliko maslahi yao binafsi au ya makundi yao.
Ndugu Mwenyekiti na Wajumbe wa Baraza la Vyama vya Siasa;
Mabibi na Mabwana;
Vyama vya siasa vina nafasi ya pekee katika majadiliano ya Bunge Maalum la Katiba na katika mchakato mzima wa kutunga Katiba mpya. Mafanikio ya mchakato huu yatategemea sana kauli, mwenendo na matendo ya vyama vya siasa. Ukweli ni kwamba vitendo na kauli za viongozi, wanachama na wafuasi wa vyama vya siasa ndivyo vitakavyojenga au kubomoa, na ndivyo vitakavyowezesha au kukwamisha mchakato huu.
Mimi nataka vyama vijenge na kuwezesha mchakato ufanikiwe na Katiba mpya ipatikane kwa wakati tunaoutarajia sote. Yaani tufanye uchaguzi wa Serikali za Mitaa na Uchaguzi Mkuu 2015 tukiwa na Katiba Mpya. Mimi naamini kwa dhati ya moyo wangu kuwa vyama vya siasa vikiamua Katiba ipatikane, itapatikana. Hivyo basi, kama vyama vya siasa vitaamua kishirikiana kwa dhati, na kwa nia njema tutapata Katiba mpya bila kelele wala mikwaruzo. Kama vyama vya siasa vitatambua kuwa tunatengeneza jambo la kutunufaisha wote, yaani nchi yetu na watu wake na siyo maslahi binafsi ya vyama vyao itakuwa hatua kubwa ya mwanzo ya kufanya kazi ya Bunge kuwa rahisi. Pia kama vyama vitakubali kuongozwa kwa nguvu ya hoja alizotoa Mjumbe na siyo Mjumbe anatokea Chama gani au kundi gani, tutapata Katiba yenye maslahi kwa taifa letu. Tutapata Katiba itakayoridhiwa na wananchi bila ya taabu.
Ninaposema hayo sina maana kuwa vyama vya siasa au Wajumbe wanaotokana na vyama wasiende Bungeni na maoni yao au na misimamo ya vyama vyao. La hasha! Nikifiria hivyo sitakuwa mkweli kwangu mwenyewe. Nitakuwa najidanganya. Ninachosema ni kwamba, pamoja na kuwa na maoni, mwongozo na misimamo ya vyama vyenu, lazima muwe na unyumbufu wa mawazo kwa kiasi fulani ili mpate nafasi ya kusikiliza hoja za wengine zinazotofautiana na zenu, kuzivumilia na kuzikubali pale ambapo kuna mantiki. Kwa lugha ya Kiingereza natoa wito wa “flexibility”. Muungwana hukubali mawazo bora na yenye ukweli ya watu wengine. Hata wengine nao wanaweza kuwa na mawazo bora kuliko yako. Muungwana ni yule anaekiri ukweli huo na yuko tayari kupokea mawazo bora ya watu wengine hata kama watu hao hawapendi. Kama tutakwenda kwenye Bunge na azimio la kupinga kila wazo litakalosemwa na mtu fulani, hatutafikia kupata Katiba mpya. Haitawezekana.
Ndugu Mwenyekiti wa Baraza la Vyama vya Siasa;
Ndugu Wajumbe;
Mtakubaliana nami kuwa Baraza hili na hasa ninyi viongozi mliokusanyika hapa leo mnayo dhamana na jukumu la kipekee la kuipatia nchi yetu Katiba nzuri yenye maslahi kwa nchi yetu na inayojali maslahi ya watu na kukubalika na watu wote. Katiba ambayo itakapotangazwa watu waseme naam, hii ni Katiba inayojali maslahi ya nchi zetu mbili zilizoungana na kuwa nchi moja miaka 50 iliyopita. Katiba inayojali maslahi ya raia wa Tanzania ndani ya Muungano na ule upande wa Muungano anakoishi au unakotoka kwa asili yake au historia yake.
Ni kwa kutambua umuhimu huu wa vyama vya siasa ndiyo maana nilitoa wito kwa vyama vya siasa kukutana na kuzungumza miongoni mwenu. Ningependa mzungumze kuhusu namna bora ya kujadili rasimu ili mwishowe tupate Katiba nzuri. Ningependa mzungumze jinsi vyama vya siasa vitakavyoshirikiana hasa kutafuta ufumbuzi wakati majadiliano yanapokuwa magumu kwa baadhi ya mambo.
Si vyema mkadhani jawabu ni kushindana mpaka mwenye nguvu ashinde. Mnaweza kushindwa wote. Na mkishindwa, mjue sote tumeshindwa na nchi imekwama. Msikubali kuifikisha nchi hapo. Tuzidi kumuomba Mola atusaidie tusifike hapo. Lakini, Mwenyezi Mungu husaidia wanaojisaidia. Na sisi tutengeneze namna bora ya kujisaidia ili Mungu akitia mkono wake mambo yanajipa. Lililoonekana kuwa zito linakuwa jepesi kama kanda la usufi.
Ndugu Mwenyekiti wa Baraza la Vyama vya Siasa;
Nawaamini nyote mliopo hapa mnaweza kutengeneza mfumo huo na taratibu hizo. Sina majibu wala maelekezo ya mfumo huo ni upi. Nimekuja kutoa rai. Nimekuja kutoa maombi. Majibu mnayo ninyi. Mimi nasubiri jibu jema kama wanavyosubiri Watanzania wengine. Nawaomba myatafakari ninayosema na myape uzito unaostahili.
Mwisho
Narudia kuwashukuru Mwenyekiti wa Baraza la Vyama vya Siasa na Msajili wa Vyama vya Siasa, kwa kunialika kuja kuongea na viongozi wa vyama vya siasa kupitia Baraza hili. Ni matumaini yangu kuwa, miaka ishirini na mbili tangu mfumo wa vyama vingi uanzishwe tena hapa nchini kwetu mwaka 1992, vyama vya siasa vimekomaa na vinaelewa nafasi na umuhimu wake katika jamii. Hivyo basi, tutegemee matokeo mema katika mkutano wenu huu wa kihistoria na mchakato utakaozaa matunda mema katika Bunge Maalum la Katiba.
Kabla ya kumaliza napenda kurudia kuwahakikishia kuwa mimi na Serikali ninayoiongoza tutaendeleza ushirikiano wetu na Baraza. Tuko tayari kuitikia wito wa kuja kuongea nanyi wakati wowote. Baada ya kuyasema maneno yangu mengi, nawatakia kila heri katika Mkutano wenu.
Mungu Ibariki Afrika!
Mungu Ibariki Tanzania!
Ahsanteni kwa kunisikiliza.