David Jairo, Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini
Dodoma,
TAARIFA zilizotolewa jana na gazeti moja la kila siku kuwa Katibu Mkuu Wizara ya Nishati na Madini, David Jairo amejiuzuru si za kweli Waziri Mkuu, Mizengo Pinda amethibitisha hilo.
Waziri Pinda amesema, kama ilivyo kwa Watanzania wengine, naye amesikia taarifa za, Jairo kujiuzulu kwenye vyombo vya habari na si kweli kwamujibu wa taratibu zilivyo.
Pinda alitoa kauli hiyo jana bungeni, alipokuwa akijibu maswali ya waandishi wa habari baada ya kuzindua maabara inayohamishika (mobile) iliyotengenezwa na Kampuni ya ML Enterprises (T) Ltd.
“Bahati nzuri umenza swali lako kwamba umesikia tetesi, hizo ni tetesi mimi sina taarifa za kujiuzulu kwake. Mimi pia leo (jana) nimeona kuna gazeti limeandika nadhani ni Jambo Leo ila mimi sijapatiwa taarifa rasmi za kujiuzulu kwake,” alisema Pinda.
Aliongeza kuwa tayari amempa taarifa, Rais Jakaya Kikwete kuhusu kitendo cha Jairo kuziandikia barua taasisi zilizo chini ya Wizara ya Nishati na Madini kuchangisha fedha kwa ajili ya kufanikisha bajeti ya Wizara hiyo kupita.
“Siwezi kusema kitu kama mnavyojua, Mheshimiwa Rais bado yupo ziarani, nilishampa taarifa akirudi atalisemea jambo hili,” alisema Pinda.
Sakata hilo linalomwandama Katibu Mkuu huyo wa Wizara ya Nishati na Madini liliiburiwa Jumatatu ya wiki hii, liliiburiwa na Mbunge wa Kilindi, Beatrice Shellukindo wakati akichangia hotuba ya Bajeti ya Wizara ya Nishati na Madini kwa mwaka wa fedha 2011/2012.
Shellukindo alisoma barua anayodai kuandikwa na Jairo kwenda katika idara za Wizara hiyo akizitaka zichange sh. milioni 50 kila moja ili kufanikisha kupita kwa bejeti ya wizara yake.