Na Yohane Gervas, Rombo
WILAYA ya Rombo ipo hatarini kukumbwa na njaa kutokana na mazao ya wakulima kukauka kufuatia ukame uliosababishwa na uhaba wa mvua katika kata zote za Wilaya ya Rombo. Kauli hiyo imetolewa jana na Kaimu Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Rombo, Protas Lyakurwa ambaye pia ni Diwani wa Kata ya Ngoyoni wakati alipokuwa akizungumza katika kikao cha kawaida cha Baraza la Madiwani.
Lyakurwa alisema ipo haja ya wakulima wilayani humo kuhamasishwa kulima mazao yanayostahimili ukame, sambamba na kuwahimiza zaidi wananchi vijijini kutunza mazingira kwani ukame huo umesababishwa na vitendo vya uharibifu wa mazingira ikiwemo ukataji holela wa miti.
Aidha alisema halmashauri hiyo imeanza taratibu za kuomba chakula cha msaada na cha bei rahisi ili kukabiliana na tatizo hilo. Naye Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Rombo, Anthoni Tesha, akichangia amebainisha kuwa kwa kipindi chote cha mwezi wa kwanza hakukuwa na mvua kabisa hali ambayo ilisababisha mazao yaliyokuwa shambani kukauka kabla hayajakomaa.
Kwa upande wake Mkuu wa wilaya ya Rombo, Elinas Pallengyo akizungumza katika kikao hicho cha madiwani, amewatahadharisha wananchi wa wilaya hiyo kutumia vizuri akiba ya chakula iliopo ili kiweze kuwasaidia katika kipindi hiki.
Aidha aliongeza kuwa wakulima wanatakiwa kujikita zaidi katika kilimo cha mazo yanayostahimili ukame kama vile mtama na mengineyo.