KIKOSI kazi cha Jeshi la Polisi cha Kudhibiti Uharamia Baharini kimekamata kilo 201 za dawa za kulevya aina heroini zilizokuwa zikiingizwa nchini kutoka Iran.
Kamishna wa Polisi, Kitengo cha Kupambana na Dawa za Kulevya, Godfrey Nzowa, alisema jana kikosi hicho kikiwa kwenye doria ya kawaida kiliona boti ambayo haikuwa na bendera wala kiashiria chochote ndipo walipoitilia shaka na kuamua kuifuatilia. Nzowa alisema kuwa mzigo huo ni mkubwa zaidi wa heroin kuwahi kukamatwa na vikosi vya doria vya Tanzania.
Alisema mara ya mwisho kwa mzigo mkubwa zaidi wa heroin kuwahi kukamatwa ilikuwa mwaka 2012 wakati zilipokamatwa kilo 70 za dawa hizo jijini Dar es Salaam. Nzowa alisema Kikosi cha Wanamaji kiliposhuku boti hiyo, kiliisimamisha na kugundua kuwa ilikuwa na watu 12.
Alisema baada ya uchunguzi wao waligundua kuwa kulikuwa na raia wanane wa Iran na wanne wa Pakistan.
“Boti hiyo ilivutwa hadi ufukweni ambako leo (jana) ilifanyiwa uchunguzi na ndipo zikakutwa na kilo 201 za heroin,” alisema Nzowa.
Nzowa alisema boti hiyo iliyosajiliwa Kunarak, Iran, ilikuwa inaongozwa na nahodha mwenye uraia wa nchi hiyo, Ayub Hot (50). Nzowa alisema kitakachofuata sasa ni kufanya upelelezi na kujua walikuwa wanataka kupeleka wapi mzigo huo, kufahamu mtandao wao na walipanga kufanya nini katika ufukwe wa Dar es Salaam.
Alisema baada ya upelelezi wao kukamilika watu hao watafikishwa mahakamani.
Naye Kamanda wa Kikosi cha Wanamaji cha Polisi, ACP Mboje Kanga alisema watu hao 12 hivi sasa wamewekwa mahabusu ya wanamaji na kikosi hicho kwa kushirikiana na Kitengo cha Kupambana na Dawa za Kulevya wataendelea na upelelezi.
Taarifa ya mwaka 2011 ya Kitengo cha Dawa za Kulevya iliyochapishwa katika ripoti ya Kitengo cha Dawa za Kulevya cha Marekani inaeleza kuwa, heroini huingia Tanzania kupitia Bahari ya Hindi ikitokea Afghanistan, Iran, Pakistan na Falme za Kiarabu.
Hapa boti ndogondogo hutumika kuzipeleka China na Bara la Ulaya kwa vifurushi vidogo vidogo.
Pia dawa za kulevya aina ya cocaine huingia Tanzania kutoka Brazil, Columbia, Peru, Trinidad na Tobago, Venezuela na Curacao, kisha hupelekwa Afrika Kusini, Ulaya, Australia na Amerika ya Kaskazini.
CHANZO; Mwananchi