SHIRIKISHO la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) limesitisha matumizi ya tiketi za elektroniki kwenye viwanja vyote vyenye huduma hiyo ili kutoa fursa ya kufanyika tathmini ya kina kabla ya kuendelea tena.
Uamuzi huo umefikiwa kwa kuzingatia sababu mbalimbali baada ya kikao kati ya Sekretarieti ya TFF na maofisa wa benki ya CRDB kilichofanyika jana (Februari 3 mwaka huu) katika ofisi za Shirikisho.
Tathmini hiyo inafanyika ili kubaini changamoto zilizojitokeza na kuzitafutia ufumbuzi kabla ya kuendelea tena na matumizi hayo, kubwa ikiwa ni hadhari iliyotolewa na vyombo vya Usalama juu ya misongamano inayotokea uwanjani kutokana na kutokuwepo mtiririko mzuri wa uingiaji.
Tayari zipo changamoto za wazi ikiwemo uelewa wa washabiki wa jinsi ya kununua na kutumia tiketi hizo, milango michache ya kuingilia uwanjani na washabiki wengi kununua tiketi dakika za mwisho hivyo kuchangia misongamano.
MTIBWA SUGAR, SIMBA KUUMANA MOROGORO
Ligi Kuu ya Vodacom (VPL) kuwania ubingwa wa Tanzania Bara inaingia raundi ya 16 kesho (Februari 5 mwaka huu) kwa mechi tano huku Mtibwa Sugar ikiikaribisha Simba kwenye Uwanja wa Jamhuri mjini Morogoro.
Kiingilio katika mechi hiyo ambayo itakuwa ya kwanza kuchezwa kwenye uwanja huo wenye uwezo wa kuchukua watazamaji 10,000 tangu uanze mzunguko wa pili wa VPL kitakuwa sh. 5,000. Jonisia Rukyaa kutoka Bukoba ndiye atakayechezesha mechi hiyo.
Mechi nyingine za ligi hiyo ni Tanzania Prisons vs Coastal Union (Sokoine, Mbeya), Mgambo Shooting vs Ruvu Shooting (Mkwakwani, Tanga), Rhino Rangers vs Oljoro JKT (Ali Hassan Mwinyi, Tabora) na JKT Ruvu vs Ashanti United (Chamazi, Dar es Salaam).
40 KUNG’AMUA VIPAJI UBORESHAJI TAIFA STARS
Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) limeteua kikosi cha makocha 40 kutoka sehemu mbalimbali, Tanzania Bara na Zanzibar ili kung’amua vipaji katika mpango wa kuboresha timu ya Taifa (Taifa Stars).
Makocha hao ambao watafanya kazi hiyo katika michuano maalumu ya mikoa wanatakiwa kuripoti katika ofisi za TFF siku ya Jumamosi (Februari 8 mwaka huu) saa 4 asubuhi kwa ajili ya kupewa maelekezo zaidi.
Walioteuliwa ni Abdallah Hussein (Kilimanjaro), Abdul Mingange (Dar es Salaam), Ali Bushiri (Zanzibar), Ali Mayay (Dar es Salaam), Ally Mtumwa (Arusha), Ayoub Selemani (Zanzibar), Boniface Pawasa (Dar es Salaam), Dan Korosso (Mbeya), Dk. Mshindo Msolla (Dar es Salaam) na Edward Hiza (Morogoro).
Elly Mzozo (Dar es Salaam), Fred Minziro (Dar es Salaam), George Komba (Dodoma), Hafidh Badru (Zanzibar), Hamimu Mawazo (Mtwara), Idd Simba (Mwanza), Jabir Seleman (Zanzibar), John Tegete (Mwanza), Juma Mgunda (Tanga) na Kanali mstaafu Idd Kipingu (Dar es Salaam).
Kenny Mwaisabula (Dar es Salaam), Khalid Abeid (Dar es Salaam), Madaraka Bendera (Arusha), Madaraka Selemani (Dar es Salaam), Mbarouk Nyenga (Pwani), Mohamed Mwameja (Dar es Salaam), Musa Kissoki (Dar es Salaam), Nicholas Mihayo (Dar es Salaam), Patrick Rweyemamu (Dar es Salaam) na Peter Magomba (Singida).
Peter Mhina (Songea), Salvatory Edward (Dar es Salaam), Salum Mayanga (Morogoro), Sebastian Nkoma (Dar es Salaam), Sekilojo Chambua (Dar es Salaam), Shaban Ramadhan (Zanzibar), Steven Nemes (Dar es Salaam), Sunday Manara (Dar es Salaam), Tiborowa Jonas (Dar es Salaam), Yusuf Macho (Dar es Salaam), Zamoyoni Mogela (Dar es Salaam),
QUALITY GROUP YAIPIGA JEKI TFF
Kampuni ya Quality Group Limited imetoa sh. milioni 10 kwa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) kwa ajili ya kuunga mkono mikakati ya shirikisho la katika kuendeleza mpira wa miguu nchini.
Mchango huo wa Quality Group utatumika katika programu mbalimbali za kuendeleza mpira wa miguu nchini ambapo tunaishukuru kampuni hiyo kwa kuunga mkono mikakati yetu.
*Imeandaliwa na Boniface Wambura Mgoyo, Ofisa Habari na Mawasiliano
Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF)